Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Kamilisheni Michoro ya Ujenzi wa Sekondari Mpwayungu kwa Wakati – Senyamule
Aug 01, 2023
Kamilisheni Michoro ya Ujenzi wa Sekondari Mpwayungu kwa Wakati – Senyamule
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule (kushoto) akiwa na Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, Mhe. Gift Msuya wakikagua eneo la ujenzi wa shule mpya ya sekondari Mpwayungu katika ziara iliyofanyika mwishoni mwa wiki, wilayani Chamwino.
Na Mwandishi Wetu

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule ameagiza Wakandarasi wanaotekeleza mradi wa ujenzi wa shule mpya ya Sekondari Mpwayungu iliyopo wilayani Chamwino kukamilisha michoro ya ujenzi huo ili kuwezesha kazi nyingine kuendelea.

Mhe. Senyamule ametoa agizo hilo mwishoni mwa wiki wakati wa ziara yake ya kikazi katika Wilaya hiyo katika Kata ya Mpwayungu ambapo ametembelea miradi kadhaa ikiwemo ujenzi wa shule hiyo, mradi wa kupambana na ujangili na biashara haramu ya wanyamapori katika mfumo wa ikolojia wa hifadhi za Ruaha (WMA) katika Kijiji cha Ndogowe na Mradi wa Kilimo cha Pamoja (BBT).

Amesema kuwa iwapo michoro hiyo itakamilika kwa wakati itatoa fursa kwa wananchi kuendelea na zoezi la kuchimba msingi ndani ya wiki moja.

Mhe. Senyamule ameelekeza Watendaji kuhakikisha wanasimamia kazi zinazowahusu ikiwemo uchimbaji wa msingi, kusogeza kokote vifusi vya mchanga ili mradi huo uweze kwenda kasi na kukamilika kwa wakati.

"Natarajia kuona uchimbaji wa msingi umekamilika ndani ya siku saba na kufanya hivyo ni ishara ya kwamba mnauhitaji wa uharaka wa maendeleo kwani serikali inahitaji kasi na ufanisi", ameeleza Senyamule. 

Aidha, amesema kuwa kiasi cha fedha zaidi ya shilingi milioni 544 zimeshatolewa kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo japo kasi ya utekelezaji ni ndogo, hivyo ametoa rai kuongeza kasi ili ifikapo tarehe10/10/2023 mradi uwe umekamilika.

Mradi huo unahusisha ujenzi wa vyumba vya madarasa 8, jengo la utawala maktaba, chumba cha TEHAMA, matundu ya vyoo vya wanafunzi 8, maabara ya sayansi 3, tanki la kuhifadhia maji moja la lita 32,000, kichomea taka na jenereta vinavyotekelezwa chini ya ufadhili wa fedha za SEQUIP. 

Eneo linalotarajiwa kujengwa shule mpya ya Sekondari Mpwayungu iliyopo wilayani Chamwino. 

Katika hatua nyingine, Mhe. Senyamule akiwa kwenye mkutano wa hadhara na wananchi wa Kijiji cha Mlazo na Ndogowe amesisitiza wananchi kujitokeza kushiriki kwa kutoa nguvu kazi kwenye ujenzi wa Shule ya Sekondari Mpwayungu.

 

"Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameelekeza kila Kata kuwa na shule ya sekondari amefanya jitihada na anaendelea kutupatia fedha kwa ajili ya kutengeneza miundombinu wezeshi kwa watoto ili maendeleo yamguse kila mmoja, hivyo tushirikiane kuunga mkono jitihada hizo." Ametoa wito Mhe. Senyamule

 

Aidha, Mhe. Senyamule amekemea vikali suala la utoro wa watoto shuleni na hatua kali za kisheria kuchukuliwa kwa wazazi wazembe kufuatilia mienendo ya watoto wao na wengine wanaobaki nyumbani kwa ajili ya shughuli za nyumbani na hivyo kupelekea watoto hao kutomaliza masomo.

 

"Tutafutilia lazima tutahakikisha mtoto mmoja mmoja anapata haki yake ya msingi ya kupata elimu na kuwachukulia hatua kali kwa wazazi watakaobainika wanachangia watoto wao kuwa watoro shuleni ", amesisitiza Senyamule 

 

Naye Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, Mhe. Gift Msuya amesema kuwa ujenzi wa shule hiyo umezingatia vigezo vyote ikiwemo umbali kwa wanafunzi na kuwataka wakazi wa kata hiyo kubadilika kwani maendeleo hayajaribiwi bali washirikiane ili kusogea mbali kuitekeleza kesho.

 

Kwa upande wake Afisa Elimu wa Mkoa wa Dodoma, Mwl. Gift Kyando amewataka Wakandarasi wanaohusika na ujenzi wa shule hiyo kutoharibu mazingira kwa kukata miti ovyo.

 

Mwalimu Kyando ametoa wito kwa wakazi wa eneo hilo kutoa ushirikiano pindi ujenzi unavyoanza sambamba na kutumia fursa zilizopo kwa muda wa utekelezaji wa miradi mbalimbali inayoendelea kutekelezwa katika kata hiyo.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi