Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Kamati ya Kudumu ya Bunge Yaipongeza TAWA kwa Ufanisi wa Minada Vitalu vya Uwindaji
Oct 27, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) kwa kuuza vitalu vya uwindaji vipatavyo 64 kwa njia ya mnada wa kielektroniki kwa ufanisi. Uuzaji huu unaifanya TAWA ifikie asilimia 79 ya vitalu vyote vya uwindaji vilivyouzwa.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Shaban Shekilindi (Mb) ametoa pongezi hizo leo Oktoba 26, 2022 Jijini Dodoma mara baada ya Kamishna Uhifadhi wa TAWA, Mabula Misungwi kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya TAWA kwa Wajumbe wa Kamati hiyo 

“Mimi pamoja na Wajumbe wa  kamati hii tunajisikia fahari sana kwa hatua hii ambayo TAWA mmeifikia kwani suala hili la kuanzishwa kwa mnada wa kielektroniki wa vitalu vya uwindaji wa kitalii lilikuwa na kelele nyingi kutoka ndani na nje ya nchi'', amesisitiza Mwenyekiti huyo Shekilindi

Ameeleza kuwa mchakato wa kuanzisha mnada wa kielektroniki wa vitalu hivyo ulipigwa vita sana na baadhi ya Wafanyabiashara wakubwa waliokuwa wametawala katika biashara hiyo, hivyo hawakutaka njia hiyo kwa hofu ya kupoteza vitalu walivyokuwa wamevimiliki kwa muda mrefu ila kutokana  na uongozi thabiti wa Wizara ya Maliasili na Utalii hawakurudi nyuma.

Kwa upande wake Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Balozi Dkt. Pindi Chana amesema zoezi hilo kwa kipindi kirefu kabla ya kuanza kutumika kwa mfumo huo lilikuwa likikumbwa na vitendo vya rushwa na ukiukwaji wa kanuni na taratibu huku akibainisha kuwa matumizi ya mfumo wa kielektroniki yameifanya biashara hiyo itulie na sasa hakuna kashfa yoyote katika vitalu vilivyouzwa

''Kwenye mnada wa kiekektoniki, wafanyabishara wa vitalu vya uwindaji wanashindana kupitia mtandao tofauti na zamani ambapo wafanyabiashara walikuwa wanakutana ana kwa ana na Watendaji wa Wizara'', amesema Balozi Dkt. Pindi Chana.

Ametumia fursa hiyo kuishukuru Kamati hiyo kwa uongozi madhubuti wa kulisimamia suala la kuanzishwa kwa mfumo huo hali iliyopelekea Serikali kuongeza mapato.

Amefafanua kuwa kwa sasa hakuna kelele kwani Wafanyabiashara wa vitalu vya uwindaji wa kitalii wameanza kuelewa lengo la Serikali na kwamba hali hiyo ya mnada imesaidia kuwaibua wafanyabishara wadogo wanaoibukia katika biashara hiyo kwa kuwa minada hiyo imekuwa huru na inampa fursa mtu yeyote kushiriki.

Katika hatua nyingine Balozi Dkt. Pindi Chana amesema vitalu 24 bado havijauzwa akieleza kuwa hivi karibuni utatangazwa mnada mwingine kwa ajili ya vitalu vilivyobaki.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi