Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

JPM: Uchaguzi Umekwisha, Tuchape Kazi
Nov 05, 2020
Na Msemaji Mkuu

Eleuteri Mangi, MAELEZO, Dodoma


Dkt. John Pombe Magufuli amekuwa Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
kuapishwa katika jiji la Dodoma mbele ya maelefu ya Watanzania na wageni waalikwa
wakiwemo baadhi ya viongozi kutoka mataifa mbalimbali Duniani kuingoza Tanzania kwa
kipindi cha pili kuanzia 2020 hadi 2025.

Akizungumza baada ya kula kiapo hicho, Rais Magufuli amesema kuwa siku kama ya leo
Novemba 5, 2015 aliapishwa katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam kulingoza taifa kwa
kwa kipindi cha miaka mitano kwa awamu iliyoishia leo tarehe 5 Novemba 2020.

“Namshukuru sana Mungu, lakini tofauti na mwaka 2015 ambapo niliapishwa jijini Dar es
Salaam kwenye Uwanja wa Uhuru, mara hii nimeapishwa Uwanja wa Jamhuri jiji hili zuri la
Dodoma ambapo ni makao makuu ya nchi, ninamshukuru sana Mungu”, alisema Rais Magufuli.

Rais Magufuli amewashukuru sana Watanzania kwa kumuamini na kumpa dhamana ya
kuliongoza taifa kwa kipindi kingine cha miaka mitano kwa kumpa ushindi mkubwa pamoja na
Chama chake cha Mapinduzi na kusisitiza huo ni ushindi wa watanzania wote.

Aidha, Rais Magufuli ameishukuru Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa kusimamia vizuri
zoezi la Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu pia amewashukuru viongozi wa dini kwa kuliombea
taifa wakati wote wa zoezi la uchaguzi, kumaliza kwa usalama na hatimaye kulifanya taifa
kuendelea kuimarika kuwa la amani na umoja.

Vile vile amevishukuru na kuvipongeza vyombo vya ulinzi na usalama kwa kufanya kazi kwa
weledi ambao umewezesha amani na usalama kutawala kwa kipindi chote cha uchaguzi.

“Kwa namna ya pekee nawashukuru na kuwapongeza sana Watanzania kwa kuonesha utulivu
mkubwa katika kipindi chote cha uchaguzi, kama mjuavyo katika baadhi ya nchi nyingine
uchaguzi umekuwa chanzo cha mogogoro, uhasama na mafarakano.

Sisi Watanzania kwa mara
nyingine tumevuka mtihani huu na kuudhihirishai ulimwengu kuwa sisi Watanzania ni wapenda
amani na tumekomaa kidemokrasia”, amesisitiza Rais Magufuli.

Katika kufikia malengo ya taifa, Dkt. Magufuli amesisitiza mara tatu “uchaguzi sasa
umekwisha” akizingatia nchi imejiwekea malengo ya kuwaletea maendeleo kwa taifa na sasa ni
muda wa kuchapa kazi kwa ushirikiano kama walivyoahidi katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM na
kuyatekeleza yote waliyoahidi pamoja na kulinda Muungano na mipaka yake, uhuru wa taifa
pamoja na Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.

Rais Magufuli ameapishwa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya
mwaka 1977 Ibara ya 42 (5) kinachobainisha kuwa “Kila Rais mteule na kila mtu atakayeshikilia
kiti cha Rais, kabla ya kushika madaraka ya Rais, ataapa mbele ya Jaji Mkuu wa Jamhuri ya
Muungano, kiapo cha uaminifu na kiapo kingine chochote kinachohusika na utendaji wa kazi
yake kitakachowekwa kwa mujibu wa sheria iliyotungwa na Bunge.”

Wakizungumza katika hafla hiyo, Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda, Rais wa Comoro
Azali Assoumani, Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe na Makamu wa Rais wa Botswana
Slumber Tsogwane wamempongeza Rais Magufuli kwa kuchaguliwa kuiongoza Tanzania na
Watanzania wote kwa kufanya uchaguzi wa amani.

Viongozi wengine waliohudhuria hafla hiyo ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza na
Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Marais Wastaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Dkt. Ali Hassan Mwinyi.

Jakaya Kikwete, Rais Mstaafu wa Burundi Sylivester Ntibatunganya,
Mabalozi wanaowakilisha nchi zao hapa nchini pamoja na Mawaziri Wakuu wastaafa, Majaji,
Mawaziri na Manaibu Waziri ambao wamemaliza muda wao wa uongozi.

Wageni wengine ni viongozi waandamizi wa Serikali viongozi wa dini, wakuu wa mashirika ya
kimataifa, wasanii kutoka Tanzania Bara na Visiwani, wanahabari na wananchi toka Dodoma na
maeneo mbalimbali nchini.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi