[caption id="attachment_3119" align="aligncenter" width="750"] Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi akiwaelezea wafanyakazi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) umuhimu wa kupima afya zao mara kwa mara japo mara moja kwa mwaka wakati wafanyakazi hao walipofika katika Taasisi hiyo leo kwa ajili ya upimaji wa afya zao.[/caption]
Na Anna Nkinda - JKCI
Viongozi wa mashirika ya Umma na Binafsi wametakiwa kujenga mazoea ya kupima afya zao mara kwa mara ili waweze kujua hali ya afya zao na ikijulikana kama wana magonjwa basi waweze kupatiwa matibabu kwa wakati.
Rai hiyo imetolewa leo na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi wakati akiongea na viongozi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) waliofika katika Taasisi hiyo kwa ajili ya upimaji wa Afya zao.
Prof. Janabi alisema baadhi ya viongozi hawana mazoea ya kupima afya zao japo mara moja kwa mwaka na inapotokea wamegundulika kuwa na tatizo la ugonjwa huwa ni kubwa na limeshaleta madhara mwilini na wakati mwingine huwa ni vigumu kutibika.
[caption id="attachment_3120" align="aligncenter" width="750"]Akizungumzia kuhusu magonjwa ya Moyo, Mkurugenzi Mtendaji huyo alisema ni muhimu mgonjwa afuate maelekezo ya jinsi ya kutumia dawa aliyopewa na daktari wake kwani kuna baadhi ya wagonjwa wamekuwa na tabia ya kuacha kutumia dawa pindi wanapojiona wamepata naafuu jambo ambalo siyo sahihi.
Akielezea jinsi ya kujikinga na magonjwa ya Moyo kwa upande wa chakula Afisa Lishe kutoka JKCI, Louisa Shem alisema ni muhimu kupunguza utumiaji wa vyakula vya mafuta kupita kiasi hasa mafuta yatokananyo na wanyama, kutumia vyakula vya nafaka zisizokobolewa.
Kupunguza unywaji wa pombe na uvutaji wa bidhaa zitokanazo na tumbaku ikiwemo sigara, kufanya mazoezi ya mwili angalau nusu saa kwa siku na kupunguza matumizi ya vyakula vyenye chumvi nyingi.
[caption id="attachment_3121" align="aligncenter" width="750"]Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Afya na Usalama Kazini kutoka NHC Dkt. Yothan Mackenzie alisema hivi karibuni walikuwa na mkutano wa Baraza la Wafanyakazi katika mkutano huo kulikuwa na mada ya ulaji na afya wakaona ni vyema mada hiyo iende sambamba na upimaji wa magonjwa mbalimbali ikiwemo ugonjwa wa Moyo.
Dr. Mackenzie alisema wanawapima viongozi hao kwa awamu hadi sasa jumla ya wakurugenzi na wakuu wa vitengo 14 wamepima na kujuwa afya zao na viongozi wengine wataendelea kupima kwani wanaamini kuwa mfanyakazi akiwa na afya njema ataweza kufanya kazi zake vizuri.
Baadhi ya magonjwa waliyopima viongozi hao ni pamoja na Moyo, tezi dume, figo na sukari.