Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imewafikia wananchi elfu 21,324 kupitia huduma ya tiba mkoba ijulikanayo kwa jina la Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan Outreach Services zilizotolewa katika mikoa 20 na maeneo ya kazi 14.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dkt. Peter Kisenge wakati wa mkutano na waandishi wa habari leo Februari 26,2025 jijini Dodoma uliolenga kueleza mafanikio ya taasisi hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita.
"Wagonjwa tuliowaona kupitia mpango huu walikuwa 21,324 na kati yao watu wazima wakiwa 20,112 na watoto 1,212 walifanyiwa uchunguzi wa magonjwa ya moyo, kati ya hao 8,873 watu wazima wakiwa 8,380 na watoto 493 walikutwa na matatizo mbalimbali ya moyo na kuanzishiwa matibabu", alisisitiza Dkt. Kisenge
Akifafanua Dkt. Kisenge amesema kati ya wagonjwa 3,249, watu wazima 2,765 na watoto 484 walikutwa na matatizo yaliyohitaji matibabu ya kibingwa na kupewa rufaa ya kuja kutibiwa katika Taasisi ya JKCI.
Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete ni Hospitali maalumu na Chuo Kikuu cha Mafunzo ya utaalamu wa matibabu ya moyo inayomilikiwa na Serikali.