Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

JKCI Yajipanga Kuwahudumia Wenye Magonjwa ya Moyo waliopatwa na Maambukizi ya Covid19
Apr 26, 2020
Na Msemaji Mkuu

  • Na Mwandishi maalum – Dar es Salaam

Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) itawahudumia wagonjwa wenye matatizo ya moyo yanayohitaji matibabu ya kibingwa walioko katika kituo cha  watu waliopata maambukizi ya virusi vinavyosababisha ugonjwa wa Corona (COVID – 19) cha Amana jijini Dar es Salaam.

Hayo yamesemwa leo na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Prof. Janabi alipotembelea kituo hicho kwa ajili ya kuona ni namna gani wataalamu wa Taasisi yake wataweza kutoa huduma kwa  wagonjwa wa moyo.

Prof. Janabi alisema licha ya Taasisi hiyo kwenda katika kituo hicho kutoa  huduma ya matibabu ya kibingwa ya moyo pia itatoa mafunzo  kwa vikundi vya watu wachache kwa wafanyakazi wa  Hospitali hiyo ambayo yatawasaidia katika utendaji wao wa kazi wa kila siku hasa katika kipindi hiki cha janga la Corona.

“Mimi pamoja na wataalamu wangu tumekuja hapa ili kuona ni jinsi gani tunaweza kushirikiana kwa pamoja katika kutoa huduma za matibabu ya moyo kwa wagonjwa. Kwani wagonjwa wa Corona ambao wanamatatizo ya moyo wanahitaji kupata huduma za matibabu walizokuwa wanazipata  kabla hawajapata maambukizi”,.

“Pia tutatoa  mafunzo katika makundi  ya watu wachache kwa wataalamu wa afya ya jinsi ya kutoa huduma kwa wagonjwa hasa wenye matatizo ya moyo”,  alisema Prof. Janabi.

Kwa upande wake Dkt. Stanley Binagi  ambaye ni msimamizi wa kituo hicho alisema baadhi ya wagonjwa waliopo katika kituo cha Amana  wanasumbuliwa na magonjwa mengine ikiwepo moyo, figo na kisukari  yanayohitaji matibabu ya kibingwa .

“Ninawashukuru Wataalamu kutoka JKCI na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ambao mmefika katika kituo hiki na kuona jinsi gani mnaweza kushirikiana na sisi katika kutoa  huduma za matibabu ya kibingwa kwa wagonjwa wa COVID -19”.

“Kupatikana kwa huduma za matibabu kutoka kwa wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kutasaidia kwa kiasi kikubwa kuokoa maisha ya wagonjwa hawa”,  alisema Dkt. Binagi.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi