Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

JKCI Kushiriki Kongamano la 8 la Dunia la Wataalam Magonjwa ya Moyo kwa Watoto Marekani
Aug 18, 2023
JKCI Kushiriki Kongamano la 8 la Dunia la Wataalam Magonjwa ya Moyo kwa Watoto Marekani
Baadhi ya Madaktari Bingwa kutoka Taasisi ya Moyo wakiendelea kutoa huduma
Na Stella Gama – Dar es Salaam

Madaktari bingwa watano wa magonjwa ya moyo kwa watoto kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wanatarajiwa kushiriki Kongamano la Nane la Dunia la Watoa Huduma za Matibabu ya Magonjwa ya Moyo kwa Watoto litakalofanyika nchini Marekani. 

Kongamano hilo linatarajiwa kuanza tarehe 28 Agosti hadi 3 septemba, 2023 ambapo jumla ya washiriki zaidi ya 4,500 kutoka nchi mbalimbali duniani watashiriki.

Akizungumza na Mwandishi wa Habari hii, Daktari bingwa wa moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Naizhijwa Majani alisema kongamano hilo hufanyika kila baada ya miaka minne ambapo mara ya mwisho lilifanyika mwaka 2017 Barcelona nchini Spain.

“JKCI iliweza kushiriki katika kongamano la saba lililofanyika nchini Spain na kujifunza kuhusu msingi wa data shirikishi wa uboreshaji wa ubora wa huduma kimataifa (International Quality Improvement Collaborative Data Base - IQIC) inayosaidia kuangalia masuala ya ubora kwenye huduma za matibabu ya moyo kwa watoto”, 

“Baada ya kujifunza tuliweza kuanzisha hapa JKCI data base hiyo na hadi sasa Tanzania ni kati ya nchi tatu za Afrika inayotumia data base hiyo inayosimamiwa na wataalam waliopo Boston”, alisema Dkt. Naizhijwa

Dkt. Naizhijwa ambaye pia ni Mkuu wa Kitengo cha Ubora wa Huduma JKCI alisema kupitia data base hiyo, JKCI inapeleka taarifa zote za upasuaji wa moyo unaofanywa, maendeleo ya wagonjwa, na aina ya upasuaji unaofanywa na kulinganishwa na wenzao wa Afrika na nchi nyingine nje ya Afrika.

Aidha, Dkt. Naizhijwa alisema katika kongamano la nane wataalam wa JKCI wameweza kutuma majalada 9 ili yaweze kutumika ambapo majalada 7 yamekubaliwa kwa ajili ya kuwasilishwa katika kongamano hilo. 

“Ni nafasi ya kipekee kwetu sisi kwani majalada hadi yaweze kukubalika kuwasilishwa katika kongamano hili la kipekee kwa watoa huduma za matibabu ya magonjwa ya moyo kwa watoto lazima yakidhi viwango vinavyohitajika”,

“Kupitia kongamano hili, JKCI inapeleka kazi zake ili ziweze kuonekana na kuitangaza Taasisi, kutengeneza uhusiano na wataalam kutoka nchi mbalimbali duniani pamoja na kufungua fursa za masomo, utafiti na kubadilishana uzoefu”, alisema Dkt. Naizhijwa 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi