Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Jengo la Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi Mtumba Kukamilika Disemba
Aug 17, 2023
Jengo la Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi Mtumba Kukamilika Disemba
Muonekano wa jengo la Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi lililopo Mtumba jijini Dodoma ambapo ujenzi wake umefikia asilimia 68.
Na Mwandishi Wetu - WUU

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya amezitaka Taasisi za Vikosi vya Ujenzi na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), wanaojenga na kusimamia ujenzi wa jengo la Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi katika Mji wa Serikali, Mtumba, jijini Dodoma kuhakikisha jengo hilo linakamilika katika ubora uliokusudiwa ifikapo Disemba mwaka huu.

Amesema licha ya kujenga majengo mazuri, taasisi hizo ziwe mfano wa upandaji miti na utunzaji wa mazingira katika miradi yote inayotekelezwa na taasisi hiyo ili kulinda mazingira na kuboresha mandhari.

Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya akitoa maelekezo kwa Mtendaji Mkuu wa Vikosi vya Ujenzi, Mhandisi Simeon Machibya (kushoto) alipokagua maendeleo ya ujenzi wa Jengo la Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Mtumba, Jijini Dodoma.

 

“Kazi yenu ni nzuri na hatua mliyofikia ya asilimia 68 inatia moyo, Serikali itahakikisha malipo yanafanyika kwa haraka ili kuwawezesha kuagiza vifaa na kuvifunga kwa wakati na hivyo kuendana na ratiba ya kukamilisha majengo hayo”, amesema Naibu Waziri Kasekenya.

Amezungumzia umuhimu wa taasisi hizo zilizo chini ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kuhakikisha miradi yote ya ujenzi inayoisimamia inakamilika kwa wakati na kwa ubunifu.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Vikosi vya Ujenzi, Mhandisi Simeoni Machibya, amemhakikishia Naibu Waziri huyo kuwa miradi yote waliyokasimiwa kuijenga itakamilika kwa wakati na hivyo kufikia malengo makubwa ya Serikali.

Mtendaji Mkuu Vikosi Vya Ujenzi, Mhandisi Simeon Machibya (kushoto) akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya (wa kwanza kulia), alipokagua maendeleo ya ujenzi wa Jengo la Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Mtumba,  jijini Dodoma..

“Tumejipanga kuhakikisha kuwa majengo ya wizara ya TAMISEMI, Mambo ya Nje na Ujenzi na Uchukuzi yanakamilika ifikapo Disemba na yanapendeza kutokana na kupandwa miti na maua ili kutunza mazingira”, amesisitiza Mhandisi Machibya.

Msimamizi wa mradi huo, Msanifu Majengo Weja Ng’olo kutoka TBA amesema ujenzi wa jengo la wizara umefikia asilimia 68 na kazi inayoendelea ni ya ukamilishaji na ufungaji wa miundombinu ya ndani na ya jengo na kujenga uzio na atahakikisha jengo la Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi linakuwa la mfano kwa kukamilika kwa muda na ubora unaotakiwa.

Meneja anayesimamia mradi wa ujenzi wa Jengo la Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Stanslaus Mkude, akielezea maendeleo ya hatua iliyofikia ujenzi wa Jengo la Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Mtumba, Jijini Dodoma

 

Zaidi ya shilingi bilioni 28 zinatarajiwa kutumika katika ujenzi huo ambao ni sehemu ya majengo 27 ya Mji wa Serikali yanayojengwa Mtumba, jijini Dodoma.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi