Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

IAA Yasaini Mkataba na TFF Kuendeleza Soka Mchini
Jan 28, 2021
Na Msemaji Mkuu

Na: Eleuteri Mangi- WHUSM, Arusha.

Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) kimesaini mkataba wa makubaliano ya ushirikiano na Shirikisho la Soka nchini (TFF) ili kuendelea kukuza michezo nchini.

Akizungumza mara baada ya utiaji saini makubaliano hayo Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Innocent Bashungwa amepongeza hatua hiyo ya Chuo cha Uhasibu Arusha kuunganisha taaluma na sekta ya michezo hatua itakayosaidia kulea, kukuza na kuendeleza vipaji katika michezo mbalimbali.

“Tutakitumia chuo hiki kama mfano kwa kufanikiwa kuunganisha mnyororo wa thamani kati ya taaluma na michezo, hatua hii ni mfano wa kuigwa na vyuo vingine nchini ili kuandaa wana taaluma na wanamichezo ambao wataleta tija kwa taifa kwa kujiongezea vipato vyao na Pato la Taifa” alisema Waziri Bashungwa.

Awali akiongea katika hafla hiyo fupi ya utiaji saini wa makubaliano hayo, Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Arusha, Prof. Eliamani Sedoyeka alisema hatua hiyo ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli katika kuendeleza mitaala ya michezo hususan somo la uongozi wa soka kwa ngazi ya Cheti, Astashahada, Stashahada, Shahada na Shahada ya Uzamili na hatimae hatua ambayo itasaidia katika uanzishaji na uendeshaji wa shule ya uongozi wa soka.

“Mwaka ujao wa masomo wa 2021/2022, tumepanga kutoa ufadhili wa masomo kwa vijana watakaofanya vizuri katika soka, na TFF watatusaidia katika kuwapata vijana hao, chuo kitawapa ufadhili wa masomo kwa upande wa ada na malazi” alisema Prof. Sedoyeka.

Kwa upande wake Rais wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), Wales Karia alisema mkakati huo wa chuo cha Uhasibu Arusha ni jawabu la kusimamia na kuendeleza wanamichezo ambao walikuwa wanapotea baada ya kumaliza kidato cha nne au cha sita.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi