Huduma za ustawi wa jamii hutolewa kwa mtu mmoja mmoja, familia/makundi mbalimbali na jamii kwa ujumla kwa lengo la kuzuia na kutatua changamoto za kijamii ili kuboresha ustawi wao kiakili, kimwili, kihisia, kijamii na kimaadili hasa kwa makundi maalum ambayo hayana uwezo wa kukidhi mahitaji ya msingi.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima leo Septemba 6, 2023 jijini Dodoma wakati akimkaribisha Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Doto Biteko kufungua kikao kazi cha Maafisa Ustawi wa Jamii wa Serikali na sekta binafsi kinachoongozwa na kauli mbiu isemayo “Malezi, makuzi kwa afya bora ya akili ni jukumu letu sote”.
“Huduma za ustawi wa jamii zinalenga kusaidia na kuwezesha makundi maalum kushiriki kikamilifu katika shughuli za ustawi na maendeleo ya kijamii. Vilevile, zinalenga kuisaidia jamii kuwa salama kwa kuwa na afua za kuzuia na kutokomeza changamoto zinazoweza kusababisha athari mbalimbali ikiwemo uhalifu”, alisisitiza Dkt. Gwajima.
Alieleza kuwa, huduma za Ustawi wa Jamii baada ya uhuru zimekuwa zikiongezeka kutoka zile za majaribio na ujenzi wa tabia na kujumuisha huduma za ustawi wa familia, watoto na malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto, huduma kwa wazee na watu wenye ulemavu, na huduma za marekebisho, ujenzi wa tabia na haki za mtoto kisheria, msaada wa kisaikolojia, ushauri na unasihi, malezi chanya, na ulinzi na usalama wa mtoto. Huduma za Ustawi wa Jamii ni mtambuka na zimekuwa zikitekelezwa na kuratibiwa kupitia Wizara za Kisekta.
Mkutano huo umeenda sambamba na Uzinduzi wa kuazimisha Miaka 50 ya Taasisi ya Ustawi wa Jamii, Uzinduzi wa Wiki ya Ustawi wa Jamii pamoja na Uzinduzi wa Mwongozo wa Taifa wa Uendeshaji, Usimamizi na Uratibu wa Mabaraza ya Usuluhishi wa Migogoro ya Ndoa 2023; Mwongozo wa Mafunzo ya Uwiano wa Kijinsia na Ujumuishwaji Jamii katika Huduma za Ustawi wa Jamii 2022; na Kiongozi cha Taifa cha Uelimishaji wa Huduma za Ustawi wa Jamii na Majukumu ya Viongozi;