HOTUBA YA BALOZI DKT. AZIZ P. MLIMA, KATIBU MKUU WA WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI KATIKA SHUGHULI YA KUFANYA USAFI KWENYE UFUKWE WA BAHARI YA HINDI, ENEO LA KIVUKONI (FERRY), DAR ES SALAAM
TAREHE 05 JUNI 2017
Waheshimiwa Mabalozi, Wakurugenzi na Makaimu Wakurugenzi kutoka Wizarani,
Wawakilishi wa Mashirika na Taasisi za Umoja wa Mataifa kwenye tukio hili;
Uongozi wa Kata ya Kivukoni ukiongozwa na Mhe. Henry Massaba, Diwani wa Kata ya Kivukoni;
Uongozi wa Mtaa wa Kivukoni ukiongozwa na Ndugu Gasper Makame, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kivukoni;
Wafanyakazi wa Wizara na Taasisi zilizo chini ya Wizara;
Wananchi wote mlioshiriki;
Waandishi wa Habari;
Mabibi na Mabwana.
Awali ya yote, napenda kuwasilisha salamu kutoka kwa Mhe. Waziri, Dkt. Augustine P. Mahiga (Mb.), pamoja na Mhe. Naibu Waziri, Dkt. Susan A. Kolimba (Mb.). Wanawasalimu sana na walitamani wajumuike nasi kwenye zoezi hili, ila kutokana na kubanwa na majukumu mengine ya kitaifa wameshindwa. Lakini wamefurahishwa na hiki tulichokifanya na wanatupongeza sana.
Wizara inawashukuru sana wote mliojumuika nasi kwenye tukio hili muhimu la kusafisha mazingira ya ufukwe huu tunapoadhimisha Siku ya Mazingira Duniani.
Maadhimisho haya kidunia yanafanyika nchini Canada, na kwa hapa Tanzania, yanafanyika kitaifa huko Butiama, Mkoani Mara, chini ya kaulimbiu: “Hifadhi ya Mazingira: Muhimili kwa Tanzania ya Viwanda”.
Kaulimbiu hii inatukumbusha kuwa tunapoelekea kwenye Tanzania ya Viwanda na Uchumi wa Kati, hatuna budi kutunza mazingira, kwani rasilimali tunazozihitaji kutimiza azma yetu hii adhimu zinapatikana kwenye mazingira na mazingira ndiyo maisha yetu. Hivyo utajiri wetu wa kwanza ni mazingira.
Mabibi na Mabwana,
Tumechagua kufanya zoezi hili la usafi kwenye ufukwe wa bahari kwa sababu tunapozungumzia utunzaji wa mazingira, suala la utunzaji wa bahari linasahaulika. Hivyo, sisi tunaikumbusha jamii kuwa bahari nayo ni sehemu ya mazingira, ni urithi wetu, ni lazima tuitunze.
Kwa bahati, wakati sisi tunafanya zoezi hili, leo hii pia kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, huko New York, dunia inakutana kujadili namna ya kuhakikisha uhifadhi wa bahari na matumizi endelevu ya rasilimali zake, ukiwa ni Mkutano wa kwanza wa Umoja wa Mataifa kuhusu suala hili.
Hivyo, ndugu wananchi wenzangu, naomba tuone umuhimu wa kutunza bahari, tunaitegemea sana kwenye uchumi wetu na maisha yetu ya kila siku, tuache kuichafua kwani ikipoteza uhai ni hasara kwetu sote.
Mabibi na Mabwana,
Mtakubaliana nami kuwa, bila kufanya zoezi hili kwa ushirikiano, tusingefanya chochote cha msingi hapa. Basi, na hili liwe funzo wakati huu tunapotekeleza Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) na Makubaliano ya Paris ambayo yote yanasisisiza uhifadhi wa mazingira. Bila ushirikiano, itakuwa vigumu kutimiza azma hiyo ya Makuibaliano ya Paris na Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs). Dunia ni yetu sote, inatutunza sote, inatukirimia sote sawa sawa, basi sote tuna jukumu la kuitunza, tena kwa ushirikiano.
Mabibi na Mabwana, Wananchi Wote Mliopo Hapa,
Kabla sijamaliza kuzungumza, napenda kutumia nafasi hii kuishukuru Ofisi ya Umoja wa Mataifa hapa nchini; Uongozi wa Manispaa ya Ilala na Kata ya Kivukoni kwa misaada yao ya hali na mali katika kufanikisha zoezi hili. Tunawashukuru sana.
Asanteni sana kwa kunisikiliza!