Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Hospitali ya Wilaya Wanging'ombe Mkombozi kwa Wananchi
Feb 01, 2024
Hospitali ya Wilaya Wanging'ombe Mkombozi kwa Wananchi
Muonekano wa Hospitali ya Wilaya ya Wanging'ombe iliyojengwa kwa fedha za Serikali
Na Jacquiline Mrisho - Maelezo

Wananchi wanaoishi katika Halmashauri ya Wanging'ombe iliyopo mkoani Njombe wameendelea kutoa pongezi kwa Serikali kwa kuwajengea na kuwawekea vifaa vya kisasa katika Hospitali ya Wilaya hiyo ambayo imewapunguzia gharama na umbali wa kufuata huduma za afya.

Wakazi wa Wanging'ombe wameyasema hayo hivi karibuni wakati wakizungumza na Maafisa Habari wa Idara ya Habari - Maelezo waliotembelea katika maeneo hayo kuchukua taarifa za maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya Serikali na kuwajulisha wananchi kupitia vyombo vya habari. 

Mwananchi Atukuzwe Kalulu amesema kuwa ujenzi wa hospitali hiyo umekuwa ni mkombozi kwao kwa kuwasaidia kupunguza gharama za huduma na usafiri kwani kabla ya kujengwa kwa hospitali hiyo walikuwa wanalazimika kwenda mbali kwa kutumia usafiri pia walikuwa wanalazimika kutibiwa katika hospitali za binafsi ambazo huduma zake ni za gharama kubwa.

"Kwa kweli tunaishukuru Serikali kwa kutuletea huduma za matibabu karibu, zimetusaidia sana kuokoa gharama na hata kupunguza vifo kwani muda mwingine wagonjwa walikuwa wanafia njiani kutokana na kukosa huduma za haraka," alisema Atukuzwe. 

Naye mwananchi ambaye alikuwa amelazwa katika hospitali hiyo, Amna Nyalusi amepongeza huduma nzuri zinazotolewa katika hospitali hiyo ambapo ameeleza kuwa tangu amefika hospitalini hapo amepata vipimo vyote na amepata dawa zote zilizokuwa zinahitajika. 

Akielezea hatua za ujenzi wa hospitali hiyo, Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Dkt. Majaliwa Chumvi amesema anaishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kazi nzuri inayoendelea kufanya na kwa jitihada za kipekee kuona kwamba kuna ulazima na umuhimu wa kujenga hospitali hiyo kwa wananchi wa Wanging'ombe ambayo imegharimu takriban shilingi bilioni 3.5 zilizoletwa kwa awamu.

"Katika awamu ya kwanza, zililetwa shilingi bilioni 1.8 zilizohusisha ujenzi wa majengo saba yakiwemo ya wagonjwa wa nje, utawala, stoo ya dawa, jiolojia, maabara, wodi ya wazazi na jengo la kufulia. Awamu ya pili ilihusisha ujenzi wa wodi tatu, wanaume, wanawake na watoto ambayo iligharimu zaidi ya shilingi milioni 500 na awamu ya tatu ilikuwa ni ujenzi wa jengo la wagonjwa wa dharura kwa shilingi milioni 390 ambapo kati ya fedha hizo, shilingi milioni 90 ilitumika kujenga nyumba ya watumishi (3 in 1)," alisema Dkt. Chumvi.

Ameongeza kuwa, awamu nyingine ilihusisha ujenzi wa majengo manne kwa jumla ya shilingi milioni 800 ikiwemo jengo la upasuaji, wodi ya upasuaji wanawake, wanaume na jengo la kuhifadhia maiti na kusisitiza kuwa, zaidi ya asilimia 90 ujenzi wa majengo hayo umekamilika.

Aidha, Hospitali hiyo imepokea vifaa vingi na vya kisasa vikiwemo vitanda, mashine ya mionzi  (X-Rays na Utra Sound) ambayo imefanya  hospitali hiyo kuimarika na inatoa huduma za maabara, wagonjwa wa kulazwa, wagonjwa wa dharura, huduma za mama na mtoto, chanjo, upasuaji wa wajawazito, huduma kwa watu wenye Virusi vya Ukimwi na Kifua Kikuu.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi