Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Hospitali ya Temeke Yafanya Upasuaji Mgonjwa Mwenye Jinsia Mbili
Oct 03, 2023
Hospitali ya Temeke Yafanya Upasuaji Mgonjwa Mwenye Jinsia Mbili
Daktari Bingwa wa upasuaji wa jumla na mfumo wa mkojo wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Temeke, Dkt. Hussein Msuma pamoja na msaidizi wake wakifanya upasuaji wa kutoa viungo vya uzazi vya kike kutoka kwenye korodani ya mgonjwa wa jinsia mbili mwenye muonekano wa jinsia ya kiume
Na Mwandishi Wetu

Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Temeke imefanya upasuaji wa kutoa viungo vya uzazi vya kike kutoka kwenye korodani ya mgonjwa wa jinsia mbili mwenye muonekano wa jinsia ya kiume. Upasuaji huo umefanywa na jopo la madaktari kutoka hospitali hiyo na limeongozwa na Daktari Bingwa wa upasuaji wa jumla na mfumo wa mkojo, Dkt. Hussein Msuma pamoja na wasaidizi wake.

Upasuaji huo umefanyika kwa mara ya kwanza katika hospitali hiyo na kwa hospitali za rufaa zilizopo Tanzania na kwamba ni moja ya mafanikio makubwa katika Sekta ya Afya Tanzania ikiwa ni moja ya jitihada ya Serikali na Wizara ya Afya kwa ujumla ni kuhakikisha Hospitali za Tanzania zina uwezo wa kutoa matibabu ya kibingwa na bingwa bobezi.

Aidha, huu ni muendelezo wa upasuaji bingwa na Bingwa bobezi katika Hospitali ya Temeke kwani ilifanikiwa kufanya upasuaji wa kutoa saratani ya figo bila kutoa figo pamoja na kutoa jiwe katika figo ambapo mafanikio haya yanatokana na uwepo wa madaktari bingwa na bingwa bobezi wenye utaalamu katika fani mbalimbali za afya katika Hospitali hiyo.

Akizungumza baada ya upasuaji kufanyika na kufanya vipimo vya sampuli zilizo tolewa katika upasuaji, Dkt. Hussein Msuma amesema kuwa Mgonjwa alifika Hospitalini akiwa na muonekano wa jinsia ya Kiume lakini ana maumbile ya ndani ya aina mbili yaani umbile la kike na la kiume, hivyo kupelekea upasuaji huo.

“Upasuaji tumefanya kwa mgonjwa aliyekuwa na muonekano wa nje wa jinsia ya kiume ila alikuwa na mifumo ya uzazi ya jinsia mbili ya kiume kwenye korodani ya kulia na yakike kwenye korodani ya kushoto,” alisema Dkt. Hussein Msuma

Alisema, kwa lugha ya kitaalam huu upasuaji unaitwa ‘scrotal hystero-salpingo-oophorectomy’ na kwa tafsiri rahisi ni upasuaji wa kutoa viungo vya uzazi vya kike kutoka kwenye korodani ya mgonjwa wa jinsia mbili mwenye muonekano wa jinsia ya kiume, ugonjwa huo unatokana na changamoto wa ukuaji wa kijinsia (ovotesticular DSD), ni ugonjwa nadra na adimu  kutokea  ambapo binadamu huzaliwa na viungo vya ndani vya uzazi (gonadi) za jinsia zote (ovari za kike na korodani za kiume)

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi