Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameendelea kukemea vitendo vya uhalifu vinavyoendelea nchini na kusisitiza kuwa serikali haitovumilia vitendo vinavyoleta machafuko na mifarakano.
Ametoa kauli hiyo leo Septemba 17, 2024 mkoani Kilimanjaro wakati akifunga Mkutano Mkuu wa Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Polisi kwa mwaka 2024 na Maadhimisho ya Miaka 60 ya Jeshi la Polisi Tanzania.
“Nawaomba Watanzania wote tusimame imara kukemea mauaji, nchi hii ina intelijensia kubwa kwa hiyo vikao vyote vinavyopanga kufanya uovu tutavijua. Tumeapa kuilinda na kuitetea Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na tutafanya kila linalowezekana kuimarisha ulinzi wa maisha na uhai wa Watanzania, hatuhitaji kuelekezwa na mtu yoyote nini cha kufanya kwani maelekezo ya Katiba yanajitosheleza”, amesema Rais Samia.
Rais Samia amefafanua kwamba, Serikali inaongozwa na falsafa ya Maridhiano, Kustahamiliana, Kubadilika na Kujenga taifa ambayo ilikuja baada ya kuona taifa limegawanyika kwa sababu ya tofauti za kisiasa na kiitikadi, falsafa hiyo ilikuja ili watu watangulize utaifa kabla ya mengine, hivyo kutekelezwa kwa falsafa hiyo siyo kuwa sheria za nchi hazifanyi kazi na kwamba falsafa hiyo hairuhusu utovu wa nidhamu kwa baadhi ya watu.
Ameongeza kuwa, kwa sababu yoyote ile, mauaji hayakubaliki na ndio maana Serikali inalaani na kutaka uchunguzi ufanyike juu ya matukio hayo kwani uhai wa mwanadamu ni jambo adhimu. Amesisitiza kuwa amani na utulivu wa nchi utalindwa kwa gharama yoyote.
Aidha, amelitaka Jeshi kuwa macho katika kipindi chote cha kabla, wakati na baada ya uchaguzi kuhakikisha yeyote anayejaribu kuhatarisha amani ya nchi kwa kisingizio cha uchaguzi anachukuliwa hatua haraka.
Akizungumza kuhusu uhalifu wa kimtandao, Rais Samia amelitaka jeshi hilo kuandaa mkakati wa kupambana na utapeli mitandaoni ili serikali ione namna ya kuliwezesha Jeshi kuwa na vyombo vya kupambana na uhalifu hasa wa njia ya mitandao na akili bandia.
Vile vile, ametoa rai kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, IGP Camillus Wambura kuongeza jitihada za kuzungumza na nchi mbalimbali ili Askari waende kujifunza wenzao wanafanya nini, pia amelisisitiza jeshi hilo kuendelea kutoa mafunzo ya ndani.