Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Hasunga Atoa Agizo kwa Bodi za Mazao Kukamilisha Kanzi Data za Wakulima Ifikapo Juni 30
Apr 12, 2019
Na Msemaji Mkuu

[caption id="attachment_42148" align="aligncenter" width="1000"] Waziri wa Kilimo Mhe. Japhet Hasunga (katikati) akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo pichani) wakati wa hafla ya kupotea msaada wa Tablets na vifaa mbalimbali vilivyotolewa na Mradi RARIS kwa kupitia UNDP na ESRF, leo Jijini Dodoma, kushoto ni Katibu Mkuu Wizara Kilimo Mhandisi Mathew Mtigumwe na kwa upande wa kulia ni Mkurugenzi Mkazi wa UNDP Natalie Boucly.[/caption]

Na Jacquiline Mrisho

Serikali imetoa agizo kwa Wakurugenzi wa Bodi za Mazao ya Kilimo nchini kukamilisha Kanzi Data ya wakulima wote itakayowawezesha wakulima hao kutambulika kwa urahisi.

Agizo hilo limetolewa leo jijini Dodoma na Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga wakati alipokuwa akipokea msaada wa vifaa mbalimbali vilivyotolewa na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) pamoja na Taasisi ya Utafiti wa Uchumi na Kijamii (ESRF) kupitia mradi wa RARIS.

Hasunga amesema kuwa muda umefika ambapo ni lazima nchi iwe na Kanzi Data ambayo itaonyesha taarifa zote za wakulima zikiwemo za kutambua idadi ya wakulima, eneo wanalofanyia kilimo,aina ya mazao yanayolimwa pamoja na kufahamu wakulima wakubwa, wakati na wadogo pia itasaidia kuweka mipango endelevu na kufanya maamuzi sahihi kwa wakulima hao.

"Imefikia wakati wakulima nao watambulike na kupewa vitambulisho, tulishakaa vikao na Bodi zote za mazao kujadili suala hilo hivyo natoa agizo kuwa ifikapo Juni 30 mwaka huu Bodi zote ziwe na Kanzi Data za wakulima isipokuwa Bodi ya Nafaka na Mazao  Mchanganyiko ambayo Kanzi Data yake itachukua muda kidogo kukamilika kwa sababu ya kuwepo kwa mazao mchanganyiko." alisema Hasunga.

Hasunga ameongeza kuwa hadi kufikia muda huu, uandikishaji wa wakulima hao unaridhisha kwani kufikia Machi, 31 mwaka  huu, uandikishaji huo umefikia takribani asilimia 72 ambapo jumla ya wakulima 1,274,337 kati ya lengo la makadirio ya wakulima 1,700,000 wamefikiwa.

[caption id="attachment_42149" align="aligncenter" width="1000"] Mratibu wa Mradi wa RARIS kutoka ESRF Dkt.Osward Mashindano akitoa taarifa ya namna Mradi wa Kilimo wa RARIS utakavyorahisha upatikanaji wa taarifa muhimu za wakulima kwa Waziri wa Kilimo Mhe. Japhet Hasunga (hayupo pichani) katika hafla ya kukabidhi vifaa mbalimbali vilivyonunuliwa kupitia mradi huo unaofadhili na UNDP pamoja na ESRF leo Jijini Dodoma.[/caption] [caption id="attachment_42150" align="aligncenter" width="1000"] Waziri wa Kilimo Mhe.Japhet Hasunga (wasita kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Wakurugenzi wa Bodi mbalimbali za mazao ya Kilimo mara baada ya kupokea msaada wa vifaa mbalimbali vilivyokuwa vikitolewa na UNDP/ESRF kupitia mradi wa RARIS uliyodhaminiwa na Shirika la Maendeleo ya UNDP, ni Mkurugenzi Mkazi wa UNDP Natalie Boucly (wa saba kulia) na Katibu Mkuu Wizara Kilimo Mhandisi Mathew Mtigumwe (wa sita kulia) leo jijini Dodoma.[/caption]

Aidha, Hasunga amefafanua kuwa ili kuhakikisha kilimo kinakuwa na tija, lazima kuhakikisha  tunaanzisha Bima ya Mazao ambayo itasaidia kilimo nchini kuwa na ulinzi hata ikitokea changamoto yoyote kwa wakulima lazima walipwe fidia kama biashara zingine zinazofanyika.

Akielezea kuhusu utekelezaji wa mradi huo, Mratibu wa Mradi, Osward Mashindano amesema kuwa mradi huo ulianza mnamo Oktoba, 2018 na unatekelezwa kila baada ya miezi mitatu ambapo kwa sasa wanaandaa utekelezaji kwa mara ya tatu.

"Kupitia mradi huu Shirika la UNDP na ESRF wametoa msaada wa vifaa kwa ajili kurahisisha utendaji kazi wa wizara hiyo vikiwemo vya vishikwambi 50, Kompyuta mpakato tatu, printa mbili pamoja na vifaa viwili vya kurekodia", alisema Mashindano.

Kilimo ndio msingi wa maendeleo, takwimu zinaeleza wazi kuwa kilimo kinatoa mchango mkubwa  kwenye maendeleo ya nchi ambapo kinachangia asilimia 28.1 ya Pato la Taifa, asilimia 30 ya fedha za kigeni. asilimia 65.5 ya ajira zote zilizopo hapa nchini, asilimia 66 za malighafi zinazohitajika viwandani pamoja na asilimia 100 ya chakula.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi