Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Hakuna Mwenye Misuli ya Kuligawa Taifa – Rais Samia
Aug 21, 2023
Hakuna Mwenye Misuli ya Kuligawa Taifa – Rais Samia
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza leo jijini Arusha wakati wa Maadhimisho ya Miaka 60 ya Kanisa la Kiinjili ya Kilutheri Tanzania (KKKT).
Na Georgina Misama – MAELEZO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema hakuna mtu mwenye nguvu za kuligawa Taifa la Tanzania wala kuharibu amani na usalama waTaifa hilo.

Rais Samia amesema hayo leo jijini Arusha wakati akiongea na viongozi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania pamoja na wajumbe wengine kutoka ndani na nje ya Tanzania na Watanzania kwa ujumla waliofika hapo kusheherekea Maadhimisho ya Miaka 60 ya KKKT yaliyofanyika leo Agosti 21, 2023 jijini Arusha.

Amesema amesikiliza kwa makini hotuba ya Askofu Mkuu wa Kanisa hilo, Dkt. Frederik Shoo ambaye aliitaja Misingi Mikuu ya Kanisa ambayo ilijumuisha Usalama, Amani, Umoja na Muendelezo wa Taifa na kwamba anawaomba viongozi wapya watakapchaguliwa kuendeleza misingi hiyo Mikuu ya Kanisa.  

“Baba Askofu, nimeisikiliza risala yako kwa umakini, niliamua kunyamaza kimya na naomba niwahakikishia kuwa, hakuna mwenye misuli na ubavu wa kuligawa taifa hili, kuuza taifa hili wala kuharibu amani na usalama tuliojenga kwenye Taifa hili,” amesema  Mhe. Rais Samia.

Akiongelea suala la utunzaji wa mazingira na mabadiliko tabianchi, Rais Samia amesema  amefarijika kuona viongozi wa dini wanasisitiza suala hilo na kwamba anatamani kuona taasisi za dini zinajiwekea mikakati mahsusi ya kupambana na uharibifu wa mazingira.

“Kwa nchi kama Tanzania ambayo asilimia kubwa tunategemea kilimo, madhara ya mabadiliko tabianchi ni makubwa sana, nawaomba wote tukawe rafiki wa mazingira kwani bila hivyo hatutaacha kuadhibiwa na athari za mabadiliko ya tabia nchi,” amesema Rais Samia.

Pamoja ma masuala ya kidini, KKKT limekuwa mstari wa mbele katika kuiunga mkono Serikali kwenye kutoa huduma za kijamii yakiwemo masula ya Afya na Elimu ambapo mpaka hivi sasa, kanisa linamiliki Hospitali 24, Vituo vya Afya 148 na Vituo 13 vya kufundishia Wahudumu wa Afya.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi