Na Veronica Simba – Dodoma
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu amesema kuwa gesi asilia inayopatikana nchini, ingali na nafasi kubwa ya kuchangia katika Pato la Taifa, tofauti na hofu ya baadhi ya watu kuwa Serikali haiipi tena kipaumbele sekta hiyo.
Alitoa kauli hiyo jana jijini Dodoma wakati akijibu hoja za wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, walizoziwasilisha katika semina maalum iliyoandaliwa na Wizara kuhusu masuala ya umeme, mafuta na gesi asilia.
Awali, wakitoa maoni na hoja mbalimbali wakati wa semina hiyo, baadhi ya wajumbe wa Kamati hiyo, walionyesha wasiwasi wao kuwa Serikali hailipi tena kipaumbele suala la gesi asilia kama ilivyokuwa miaka kadhaa iliyopita.
“Serikali haijabadili msimamo na mtazamo wake kuhusu gesi asilia hata kidogo. Ndiyo maana Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limepewa dhamana ya kufanya kazi kibiashara ambapo pamoja na mambo mengine, linashughulika na biashara ya gesi ili kukuza mchango wake katika Pato la Taifa,” alifafanua Naibu Waziri.
Akifafanua zaidi, alisema kwamba, miradi mbalimbali ya gesi asilia inaendelea hivi sasa ambayo ni pamoja na uunganishaji wa gesi katika kiwanda cha saruji cha Dangote, katika viwanda vikubwa vilivyopo Mkuranga pamoja na kuunganisha majumbani.
Aidha, alisema, Mpango Mkakati wa matumizi ya gesi asilia umeainisha ni kiwango gani cha gesi kitatumika katika viwanda vya mbolea, viwanda vya kawaida na katika matumizi ya majumbani.
Hata hivyo, Naibu Waziri alibainisha kuwa, umuhimu wa gesi asilia kwa Taifa, haundoi umuhimu wa vyanzo vingine mbalimbali vya nishati ambavyo Tanzania imejaaliwa kuwa navyo vikiwemo vya maji, jotoardhi, upepo, tungamotaka na kadha wa kadha.
“Lengo la Serikali ni kuhakikisha tunavitumia ipasavyo vyanzo vyote hivyo tulivyonavyo, kila kimoja kwa nafasi yake ili tuweze kuzalisha nishati ya kutosha itakayoleta tija kwa wananchi na Taifa letu kwa ujumla.”
Akizungumzia Miradi ya uzalishaji umeme ambayo kwa sasa Serikali imeelekeza nguvu zaidi, alisema ni pamoja na ule wa kuzalisha umeme kwa kutumia maporomoko ya maji ya Mto Rufiji, ambao alisema, ukikamilika utaleta tija kubwa kwa Taifa.
Kuhusu hofu inayozungumzwa na baadhi ya watu kuwa, utekelezaji wa Mradi huo utaleta changamoto nyingi; Naibu Waziri aliwahakikishia wawakilishi hao wa wananchi kuwa, Taarifa ya wataalam kuhusu Athari za Kimazingira (EIA), imebainisha kuwa faida za Mradi endapo utatekelezwa ni kubwa sana ukilinganisha na changamoto, ambazo ni chache.
Semina hiyo kwa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini ilikuwa ya siku mbili na ilihitimishwa jana, Septemba 9, 2018.