Na shamimu Nyaki - WUSM
Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Pauline Gekul amewasihi Watanzania kuiunga mkono timu ya taifa ya watu wenye ulemavu, Tembo Worriors katika mechi yake na timu ya taifa ya Japan baadae leo ili kufuzu hatua ya robo fainali ya michezo hiyo katika Kombe la Dunia nchini Uturuki.
Mhe. Gekul ametoa rai hiyo leo Oktoba 05, 2022 jijini Tanga alipokua anatoa salamu za wizara katika ufunguzi wa michezo ya Wizara, Idara, Wakala, Mikoa na Taasisi za Serikali ( SHIMIWI), ambapo amesema timu hiyo tayari imefuzu hatua ya 16 bora.
"Tanzania tumeendelea kufanya vizuri kwenye michezo, na mwaka huu timu zetu za Serengeti Girls inashiriki kombe la Dunia nchini India na timu ya Kabbadi wanawake na wanaume wamefuzu kombe la Dunia litakalofanyika Januari 2023, tunamshukuru sana Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa uwezeshaji wa timu hizi," amesema Mhe.Gekul.
Ameongeza kuwa, michezo ya SHIMIWI inasaidia kuboresha afya, kufahamiana, kujenga ushirikiano na kukuza vipaji katika zama hizi ambazo michezo ni ajira Duniani, huku akisisitiza Watumishi hao wanashiriki mazoezi ya kila mwisho wa mwezi ili kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza.
Mhe. Gekul amesema Serikali inaendelea kuboresha miundombinu ya michezo kwa kutenga fedha kila mwaka wa fedha.
Michezo hiyo mwaka huu inaongozwa na kauli mbiu "Michezo Hupunguza Magonjwa Yasiyoambukiza na Kuongeza Tija Mahala pa Kazi, Kazi Iendeleee" na imeshirikisha wanamichezo 2,510 kutoka wizara 27, mikoa 18 na Idara 18.