[caption id="attachment_33702" align="aligncenter" width="750"] Mkemia Mkuu wa Serikali, Dkt. Fidelice Mafumiko (aliyesimama) akitoa hotuba wakati wa kufunga mafunzo ya siku tatu ya Usimamizi Salama wa Kemikali kwa wahitimu wa masomo ya Shahada ya Uhandisi wa Sayansi ya Madini na Uchakataji Madini (B.Sc. Metallurgy and Minerals Processing Engineering) wa Chuo cha Sayansi ya Ardhi (CoES), Chuo Kikuu cha Dodoma, yaliyofanyika mkoani Dodoma.[/caption]
Na Jacquiline Mrisho .
Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) imejipanga kuanza kutoa mafunzo endelevu ya matumizi ya kemikali katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) ili kuongeza uelewa wa matumizi bora ya kemikali hizo.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dodoma na Mkemia Mkuu wa Serikali Dkt. Fidelice Mafumiko alipokuwa akifunga mafunzo ya siku tatu juu ya matumizi ya kemikali kwa jumla ya wanafunzi 40 wa Chuo Kikuu cha Dodoma wanaosoma masomo ya Uhandisi wa Uchenjuaji Madini.
Dkt. Fidelice amesema kuwa moja ya kazi za Mamlaka hiyo ni kutoa elimu kwa wadau wa kemikali ili kuwawezesha kufahamu matumizi bora ya kemikali yakiwemo ya uzalishaji, usafirishaji, uuzaji pamoja na uhifadhi wa kemikali.
[caption id="attachment_33703" align="aligncenter" width="750"]"Mafunzo ya masuala ya kemikali ni ya muhimu hasa ukizingatia nchi yetu inaelekea katika uchumi wa viwanda ambapo matumizi ya kemikali yataongezeka hivyo tunajipanga kuweka mikakati bora ambayo itatuwezesha kutoa mafunzo ya kemikali chuoni hapa kwa wanafunzi wanaosoma kozi zinazohusisha matumizi ya kemikali", alisema Dkt. Mafumiko.
Dkt. Fidelice ameongeza kuwa uanzishwaji wa mafunzo ya kemikali katika chuo hicho ni mlango wa mahusiano ya kitaaluma kati ya Mamlaka na chuo jambo ambalo litasaidia kukuza uelewa juu ya matumizi ya kemikali.
Mkemia Mkuu wa Serikali ametoa rai kwa wanafunzi hao kuwa mabalozi wa matumizi bora ya kemikali katika jamii zao pamoja na kuwa wataalam wenye uelewa na weledi juu ya matumizi ya kemikali.
[caption id="attachment_33704" align="aligncenter" width="750"]Kwa upande wake Mkuu wa chuo cha Sayansi ya Ardhi (CoES) Prof. Willium Mwegoha amesema kuwa wanafunzi wa kozi hiyo ni wadau wakubwa wa kemikali kwa sababu kazi zao zinahusisha matumizi ya kemikali.
"Tangu kozi hii ianze hatujawahi kupata mafunzo ya aina hii hivyo tunaomba yaendelee na siku zijazo kwani yana umuhimu mkubwa kwa wanafunzi hawa", alisema Prof. Mwegoha.
Akiwawakilisha wanafunzi wenzie, Hemed Omary amesema kuwa mafunzo hayo yameongeza uelewa wa matumizi ya kemikali hasa katika masuala ya sheria ya usimamizi na udhibiti wa kemikali pamoja na madhara ya kemikali kwa afya na mazingira.