Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Filamu Yazalisha Ajira 30,000 Mwaka Uliopita
Oct 04, 2022
Na Jacquiline Mrisho


Na Ahmed Sagaff, Dodoma


Tasnia ya filamu Tanzania imezalisha ajira 30,000 mwaka 2021 na kufanikiwa kupunguza makali ya maisha kwa vijana wa kitanzania.


Akizungumza na Watanzania kupitia vyombo vya habari leo jijini Dodoma, Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania, Dkt. Kiagho Kilonzo amesema takwimu hizo ni za kuanzia Januari hadi Desemba.


“Kiasi hicho ni ongezeko la nafasi 5,000 kutoka 25,000 kiasi cha ajira zilizozalishwa mwaka 2020,” ameeleza Dkt. Kilonzo.


Amesema idadi ya ajira zilizozalishwa zimetokana na ongezeko la uwekezaji kutoka sekta binafsi.


“Kwa mfano mwaka 2021, kampuni ya Azam Media iliwekeza takriban Shilingi bilioni nne kwenye filamu pekee, ikiwa ni ongezeko la Shilingi bilioni moja kutoka mwaka 2020 ambapo iliwekeza Shilingi bilioni tatu katika ununuzi wa filamu na udhamini kwenye uandaaji wa filamu.


“Mwaka 2020 kampuni ya Multichoice Tanzania iliwekeza takriban Dola za Marekani milioni tatu kudhamini uandaaji na ununuzi wa filamu za kitanzania,” amearifu Dkt. Kilonzo.


Juhudi hizo ni sehemu ya utekelezaji wa Ibara ya 241 ya Ilani ya CCM (2020-2025) inayoielekeza Serikali kuboresha sanaa nchini ili kuwezesha upatikanaji wa fursa zaidi za ajira.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi