Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

EU Yamwaga Bilioni 265 Kuinua Kilimo Tanzania
Oct 03, 2018
Na Msemaji Mkuu

Na Mwandishi Wetu

Jana, 02 Oktoba, 2018, Umoja wa Ulaya (EU), umeipatia Tanzania ruzuku ya Euro 103.5, sawa na shilingi bilioni 265 kwa ajili ya kuendeleza kilimo kwa kuongeza mnyororo wa thamani na masoko katika mazao ya matunda na mbogamboga pamoja na mazao ya chai na kahawa.

Kupitia mradi uliopewa jina la AGRI-Connect, Jumuiya ya Ulaya itatoa Euro 100m na washirika wa umoja huo watachangia kisi cha Euro 3.5m.

Malengo ya mpango huo ni kuhakikisha wakulima wanakuwa na soko la uhakika la mazao yao, kukuza ajira kupitia sekta ya kilimo, kuchochea uwekezaji kwenye kilimo pamoja na kuimarisha usalama wa chakula na lishe.

Aidha, makubaliano hayo yaliyotiwa saini kati ya Balozi wa EU hapa nchini Balozi Roeland Van De Geer na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James, yanalenga kuongeza uzalishaji wa mazao husika, kuimarisha upatikanaji wa masoko ya uhakika, na kuondoa changamoto ya upotevu wa mazao wakati na baada ya mavuno.

Katika kukabiliana na upotevu wa mazao wakati na baada ya mavuno, mradi huo unalenga kuimarisha miundombinu ya barabara maeneo ya vujijini ili ziweze kupitika wakati wote.

Hatua hiyo pia imelenga kuongeza kiwango cha mazao kwa tani kitakachosafirishwa pia nje ya nchi na kuongeza mapato.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James, ameushukuru Umoja wa Ulaya-EU, kwa msaada huo utakaochochea maendeleo ya sekta ya kilimo nchini na kupunguza umasikini.

James amebainisha kuwa Umoja huo wa Ulaya, tangu ushirikiano wake na Afrika, Karibian na Pasifiki (ACP) uliposainiwa mwaka 1975, Tanzania imenufaika kwa kupokea msaada wa kiasi cha Euro 2,394m sawa na zaidi ya sh. 5.5 trilion na kiasi kingine cha mkopo wenye masharti nafuu kutoka Benki ya Uwekezaji ya Ulaya cha Euro 270,865,644.

Alisema kuwa fedha hizo zimewekezwa kwenye miradi ya ujenzi wa miundombinu ya barabara, viwanja vya ndege, umeme, biashara, kilimo, mazingira, mabadiliko ya tabianchi pamoja na uchumi na sera.

Bw. Doto James alieleza kuwa msaada huo umekuja wakati muafaka kuongeza nguvu katika mpango wa kuendeleza kilimo (ASDP II), uliozinduliwa na Mhe. Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli hivi karibuni.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi