Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

EREA Yajitambulisha kwa Dkt. Kalemani
Aug 18, 2021
Na Jacquiline Mrisho

Zuena Msuya, Dodoma,

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani ameahidi kufanya kazi kwa ushirikiano na Muungano wa Taasisi za Udhibiti wa huduma za Mafuta na Umeme kwa nchi sita (6) za Afrika Mashariki (EREA) mara tu taasisi hiyo itakapokamilisha taratibu zinazotakiwa.

Dkt. Kalemani alisema hayo wakati wa mazungumzo na Katibu Mtendaji wa EREA, Dkt. Geoffrey Mabea na ujumbe wake, walipofika ofisini kwa Waziri huyo jijini Dodoma, Agosti 17, 2021,  kujitambulisha, kwa lengo la kueleza majukumu yao juu ya muungano huo na namna inavyofanya kazi kwa nchi husika.

Dkt. Kalemani alisema kuwa Wizara ya Nishati, iko tayari kushirikiana na EREA katika kutekeleza majukumu yake kwa manufaa ya nchi za Afrika Mashariki, kwa kuwa nchi hizo zimekuwa zikishirikiana katika mambo mbalimbali ya kimaendeleo.

Aidha, aliitaka taasisi hiyo kukamilisha rasimu ya Mkataba wa utekelezaji wa majukumu yake ili isambazwe kwa nchi husika ili kila moja iweze kutoa maoni yake.

Sambamba na hilo, alizishukuru taasisi za kifedha hasa Benki ya Dunia na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa kufadhili wa uundwaji wa Taasisi hiyo na kuwa bega kwa bega katika kukuza Sekta ya Nishati nchini.

Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa EREA, Dkt. Geoffrey Mabea, aliipongeza Tanzania kupitia Wizara ya Nishati kwa kuwa nchi ya tatu Afrika katika uthibiti wa masuala ya nishati.

Vilevile alieleza kuwa taasisi hiyo ina malengo makubwa matatu, moja likiwa ni kuwezesha muunganiko wa kisera katika masuala ya nishati kwa nchi wanachama katika kazi za udhibiti wa bei za mafuta na umeme.

Pia kufanya tafiti za kisera hususani katika sekta ya nishati na kuwezesha ushirikishwaji wa taarifa kwa nchi za Afrika Mashariki na kujenga uwezo kwa Taasisi za Udhibiti kwa nchi wanachama pamoja na washirika wote katika sekta ya nishati.

Dkt. Mabea alitaja nchi wanachama katika taasisi hiyo kuwa ni Tanzania, Kenya, Rwanda, Burundi, Uganda na Sudani Kusini ambapo Makao Makuu ya taasisi hiyo yapo mjini Arusha, na kwamba ilianzishwa rasmi mwaka 2009.

Hata hivyo alieleza kuwa, tayari imeandaliwa rasimu ya Mkataba wa Makubaliano ambao utasambazwa kwa nchi wanachama ili waweze kutoa maoni na Mkataba huo ukikamilika utapelekwa kwa kila nchi wanachama ili uweze kusainiwa.

Lengo la mkataba huo ni kusaidia kuridhia ujenzi wa Chuo cha Udhibiti kinachotarajiwa kujengwa Nchini Tanzania katika Jiji la Arusha.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi