Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Epicor 10.2 Kuongeza Uwajibikaji na Tija
Jun 07, 2018
Na Msemaji Mkuu

Ndugu Emmanuel Richard mhasibu wa wa halmashauri ya Wilaya ya Bariadi, akifanya mahojiano na Atley Kuni Afisa habari OR TAMISEMI jijini Mwanza wakati wa Mafunzo ya Epicor 10.2 (Picha na Gladys Mkuchu-PS3).

Na: Atley Kuni- OR TAMISEMI

Waweka hazina pamoja na wahasibu kutoka katika halmashauri za mikoa ya Mwanza na Simiyu wanaoendelea na mafunzo ya mfumo wa Uhasibu na uandaaji wa taarifa (Epicor 10.2) wamekiri kuwa mfumo huo utawaongezea tija katika utendaji wao wa kila siku.

“Hivi sasa jukumu langu kubwa litakuwa kuhakikisha taarifa zangu za ukusanyaji mapato kutoka katika mfumo wa LGRCIS zinakuwa sahihi na  mfumo kwa namna ulivyo tengenezwa utakuwa na uwezo wa “ku-post” wenyewe kila inapofika saa 6.00 za usiku” anasema Rahabu Daudi ambaye ni mhasibu wa Halmashauri wa Wilaya ya Busega.

Maelezo hayo ya Rahabu Daudi hayatofautiani sana na  Kessy Mpakata Mweka hazina katika Jiji la Mwanza yeye alisema “Mfumo wa Epicor 10.2 sasa unaunganishwa na mifumo mingine kama PlanREp iliyoboreshwa, LGRCIS, FFARS na GoTHoMIS ambayo itakuwa ni msaada mkubwa katika kuongeza tija na ufanisi, kufikia mpaka katika ngazi za kutolea huduma”

Waweka Hazina hao wanasema kuwa, utaratibu wa kuanza kutumika kwa mfumo huo wa Epicor 10.2 itasaidia hata katika suala zima la urejeshwaji wa masarufu kwa wakati, kwakuwa mfumo hautaruhusu mtumishi kuchukua masarafu mapya kabla yakufanya marejesho ya awali.

“Hivi sasa (imprest) masarufu yote yatapita katika mfumo wa (Epicor 10.2) kwa maana hiyo kabla yakuchukua masarufu mapya mfumo utakuuliza juu ya masarufu ya awali kama hujafanya marejesho mfumo hauta kukubalia, hali hii itakuwa ni ahueni katika utendaji na itasaidia hata kupunguza hoja za ukaguzi” alisema Mpakata.

Jambo jingine ambalo limepatiwa ufumbuzi na mfumo huu ni uhamishaji fedha kutoka fungu moja kwenda fungu jingine (realocation), jukumu kubwa litakalobakia mikononi mwa mtunza hazina ni kusaini yaani  (Approve) na hivyo kuondosha malalamiko mengi miongoni mwa waweka hazina na kukomesha urasimu usikuwa wa lazima, anasimulia Mpakata.

 Kwa upande wake Journey Kivaula, ambaye ni mweka hazina katika Halmashauri ya wilaya ya Maswa  anasema katika mfumo wa sasa, mipango na bajeti itakwenda na uhalisia kutokana na kwamba vifungu  vitakavyokuwa vimebajetiwa ndivyo hivyo hivyo vitakavyotumika. Kwa  utaratibu wa sasa wakuhamisha fedha za matumizi X kuhamishia kwenye matumizi Y, hilo halitakuwepo na kwa hali hiyo kadhia hiyo haitakuwepo tena, shabaha nikuondokana na hoja za mara kwa mara lakini pia kupunguza matumizi ambayo hayakubajetiwa.

 Bi. Zubeda Nkuba Mhasibu wa  Matumizi kutoka  Halmashauri ya manispaa ya Jiji la Mwanza, akielezea faida za mfumo wa Epicor 10.2 na maboresho muhimu yaliyofanyika (Picha na Atley Kuni- OR TAMISEMI)

 Kwa upande wake mhasibu kutoka Jijini Mwanza, Zawadi Jabri, alisema Epicor 10.2 ni mfumo wenye kasi na uliongeza ufanisi kwakuwa ni (Web-based) tofauti na ilivyokuwa hapo awali kwenye Epicor 9.5 na mifumo mingine mingine iliyotangulia ambayo ilikuwa na ukomo (limit) sambamba na kubaguliwa kwa baadhi ya vitu, Epicor 10.2 kwa sasa itapatikana sehemu yoyote na hivyo kurahisha utendaji wa kazi zao za kila siku.

Sambamba na maboresho hayo Zawadi alisema suala la kuunganishwa na mifumo mingine kama FFARS ambayo inaanzia ngazi ya msingi za kutolea huduma ni neema nyingine itakayochagiza ubora wa mfumo huo pamoja na kuharakisha kasi ya maendeleo kwa wananchi tunao wahudumia.

“Kuunganishwa kwa mfumo wa FFARS, itatusaidia sisi wahasibu kujua mapato kutoka ngazi ya msingi ya kutolea huduma kama vituo vya afya na Shule na itaturahisishia kujua mapato na matumizi ya mfumo huo wa FFARS” aliongeza Zawad Jabri.

Wakizungumzia juu ya maboresho ya msingi katika mfumo huo, wahasibu wawezeshaji kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI, Stanslaus Msenga na Melkzedek Kimaro katika kituo cha Mwanza, walisema mfumo huo kwa sasa utaunganishwa na mifumo mingine yote ya msingi ya usimamizi wa fedha na hivyo utakuwa na uwezo wakuwafanya walipaji kama mabenki kulipana kwa njia ya kieletroniki ya (TISS) lakini pia mfumo huo utahusisha muundo mpya wa uhasibu wa (New Chart of Account) pamoja na Kasma mpya ya 2014 (GFS).

Akitoa rai kwa wataalam wa fedha wanaoendelea na kikao katika kituo cha Mwanza, Mtaalam mshauri kutoka PS3 Bw. Ng’wananyamate Langalanga Mgengeli Mihayo, alisema kutokana na hitilafu nyingi zilizosababishwa katika kipindi cha nyuma kama uwepo hati zenye mashaka au hati chafu na makandokando mengine kupitia Epicor 10.2 itasaidia kusuluhisha ambapo cha msingi wazingatie elimu hii wanayopewa na kuieneza huko kwenye halmashauri zao. “Rai yangu kwa Wataalam wa fedha ni kuwa, wazingatie mafunzo hayo kwa umakini ili yaweze kuwaongezea weledi katika utendaji wao hususan suala zima la ukusanyaji mapato kwa njia ya mifumo na kutolea taarifa sahihi kupitia mifumo yote ya msingi iliyopo kwenye Halmashauri” Alisema Mgengeli.

Wakihitimisha mahojiano hayo, wataalam hao wa fedha hawakuacha kuushukuru mradi wa uimarishaji wa mifumo ya sekta ya umma (PS3) pamoja na Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa jinsi wanavyo endelea kutafuta mbinu mbali mbali kwa mustakabali wa kuboresha mifumo ya umma na kuwaletea maendeleo watanzania.

“Watanzania nilazima tuelewe hakuna mabadiliko yanayokuja kirahisi, tukisikia nchi zilizo endelea ni kwamba, wananchi na viongozi walikubali mabadiliko ya kweli, na Rais wetu Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli na Serikali yake huko ndipo wanapo taka na sisi tufike, hivyo kila mmoja wetu awe tayari kumuunga Mkono Mhe. Rais na watendaji wake wote kwa manufaa ya Taifa letu” alihitimisha Mpakata

Mafunzo ya juu ya mfumo wa Epicor 10.2 yanaendeshwa katika vituo mbalimbali nchini yanatarajia kuwafikia watumishi wa umma 950 wa kada za uhasibu kutoka Mamlaka za Serikali za Mitaa 185 na yanaendesha na Ofisi ya Rais TAMISEMI pamoja na Serikali ya Marekani kupitia mradi wa USAID wa Uimarishaji wa Mifumo ya Sekta za Umma (PS3) kwa Mikoa ya Mwanza, Kagera, Dodoma, Iringa, Mtwara na Mbeya.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi