Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Eneo la Mradi wa kuzalisha Umeme wa Maji ya Mto Ruhudji Lakaguliwa.
Jan 13, 2021
Na Msemaji Mkuu

Na Zuena Msuya - Njombe

Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Leonard Masanja ameiongoza timu ya Wataalamu iliyoundwa kutoka Wizara ya Nishati pamoja Shirika la Umeme nchini (TANESCO) kukagua eneo la mradi wa kuzalisha Umeme kwa kutumia maporomoko ya maji ya Mto Ruhudji.

Timu hiyo iliundwa mahsusi kwa ajili ya kusimamia kazi za awali kabla ya kuanza rasmi kwa utekelezaji wa ujenzi wa mradi huo ambapo pia itashirikisha Taasisi na Wizara mbalimbali za serikali.

Ziara hiyo ilifanyika Januari 12, 2021 ikiwa na lengo la kukagua na kuona jiografia ya eneo husika lililopo kati ya Kijiji cha Itipula na Lupembe, wilayani Njombe mkoani Njombe.

Kwa mujibu wa Mhandisi Masanja, mradi huo unatarajiwa kuzalisha takribani Megawati 358 ambazo zitaingizwa katika Gridi ya Taifa pindi mradi huo utakapokamilika.

Katika utekelezaji wa mipango ya Serikali, mradi huo utaanza kujengwa Mwezi Julai 2021 na utatekelezwa ndani ya kipindi cha miezi 36.

Mhandisi Masanja aliwatoa hofu watanzania kuwa endapo mradi huo utalazimika kuchukuwa baadhi ya maeneo ya wakazi wanaozunguka eneo la mradi, sheria na taratibu za nchi zitafuata ili kila mmoja apate haki yake ikiwemo kulipa fidia.

“Mradi huu ni muhimu sana kwetu na umekuja wakati sahihi kwa kuzingatia uchumi wa viwanda, hivyo kuongeza kasi ya uwekezaji katika ujenzi viwanda vipya, kuongeza na kuboresha uzalishaji katika viwanda vilivyopo sasa,

Vilevile kuendelea kutekeleza azma ya serikali ya kuwa na umeme wa kutosha, wa uhakika, wa kutosha na wa gharama nafuu nchi nzima”, alisema Mhandisi Masanja.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme nchini (TANESCO), Dkt. Tito Mwinuka alisema kuwa shirika hilo limeupokea mradi huo na kwamba wako tayari kuanza utekelezaji wa ujenzi wake kulingana na taratibu na miongozo ya Serikali.

“TANESCO tuna uzoefu katika kutekeleza miradi mikubwa na midogo ya kuzalisha umeme ikiwepo ya maji, kama vile Mtera, Kidatu, Kihansi na huu mwingine mkubwa kabisa wa Julius Nyerere, pia tuna ile ya gesi kule Kinyerezi, niwatoe hofu watanzania kuwa mradi huo utakamilika kwa wakati na endapo kuna maeneo ya watu katika eneo la kuzunguka mradi sheria na kanuni za nchi zitafuata ili kila mmoja aweze kupata haki yake”, Alisisitiza Dkt. Mwinuka.

Ikumbukwe kuwa Januari 8, 2021, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli alikutana na kufanya mazungumzo na Mjumbe wa Baraza la Taifa na Waziri wa Mambo ya nje ya China, Wang Yi ambaye alifanya ziara hapa nchini.

Katika mazungumzo yao pamoja na mambo mengine Rais Dkt. Magufuli aliomba ufadhili wa ujenzi wa miradi miwili ya kuzalisha Umeme kwa Kutumia Maporomoko ya Maji ya Mto Ruhudji na Rumakali kutoka Serikali ya China

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi