[caption id="attachment_15085" align="aligncenter" width="750"] Meneja wa Forodha Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), bandaroi ya Dar es Salaam, Bw. John Micah, akifafanua jambo kwa Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (hayupo pichani), alipofanya ziara ya kushitukiza bandarini, Jijini Dar es Salaam.[/caption]
Benny Mwaipaja, WFM, Dar es Salaam
WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, amefanya ziara ya kushitukiza katika Kituo cha Forodha Bandarini, kilichoko katika Bandari ya Dar es Salaam na kuiagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA, kufanya mabadiliko makubwa ya watumishi walioko katika idara ya upimaji na ukaguzi wa mizigo baada ya kubainika kuwa baadhi yao wanajihusisha kwa namna moja au nyingine na upotevu wa mapato ya Serikali.
Dokta Mpango ametoa muda wa siku saba kwa TRA kumpa taarifa kamili ya utekelezaji wa maagizo hayo, ikiwemo kuwahamisha watumishi wote waliokaa muda mrefu kwenye eneo hilo la upimaji na ukaguzi wa mizigo ili kuongeza ufanisi wa ukusanyaji mapato ya Serikali katika Bandari hiyo.
[caption id="attachment_15088" align="aligncenter" width="750"] Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (wa pili kushoto) akitoa maelekezo kwa Maafisa waandamizi wa Mamlaka ya mapato Tanzania-TRA, alipofanya ziara ya kushitukiza bandari ya Dar es Salaam na kuagiza kitengo cha ukaguzi na upimaji wa mizigo bandarini kifumuliwe baada ya watumishi wake kutofanyakazi ya kukusanya mapato ya Serikali ipasavyo.[/caption]Ameshangazwa na kitendo cha Mapato katika Bandari ya Dar es Salaam kutoongezeka licha ya juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano, kuboresha Bandari hiyo kutokana na baadhi ya watumishi wasio waaminifu kushirikiana na wafanyabiashara wasio waaminifu kukwepa kodi ya serikali.
“Pamoja na kuwepo kwa mitambo ya kukagua mizigo (Scanners), baadhi ya bidhaa zinakadiriwa kodi ndogo ikilinganishwa na thamani ya mizigo huku mizigo mingine ikiwa si ile iliyotajwa kuwemo kwenye makontena na hupitishwa na watumishi wasio waaminifu” alisisitiza Dokta Mpango.
Aidha, Waziri huyo wa Fedha na Mipango ameuagiza ungozi wa TRA kuhakikisha kuwa wanaongeza mapato katika bandari ya majahazi kutoka wastani wa mapato ya shilingi bilioni 3.5 kwa mwezi hadi shilingi bilioni 5, kulingana na malengo yaliyowekwa baada ya kubainika kuwa kuna ukwepaji mkubwa wa mapato ya Serikali katika eneo hilo.
[caption id="attachment_15091" align="aligncenter" width="750"] Afisa Kitengo cha Bandari Majahazi, Bw. Mahmood Makame, akifafanua jambo mbele ya Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (kushoto) kuhusu changamoto ya elimu kuhusu masuala ya kodi kwa wateja wanaotumia Bandari ya Dar es Salaam, alipofanya ziara ya kushitukiza katika ofisi hiyo. (Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha na Mipango)[/caption]Dokta Mpango ameuambia uongozi huo wa Mamlaka ya Mapato nchini TRA kuhakikisha kuwa Bandari ya Majahazi ianze mara moja kutumia mfumo wa kukusanya mapato ujulikanao kama TANSIS ili kudhibiti mianya ya ukwepaji kodi.
Aidha, ameviagiza vyombo vya dola kuwachunguza watumishi wote wakiwemo wa ngazi za juu katika idara ya forodha bandarini na kuwachukulia hatua kali wale wote watakao bainika kujihusisha na vitendo vyovyote vinavyoikosesha Serikali mapato yake.