Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Dkt. Tizeba Aagiza Bodi ya Sukari Kupima Sukari Yote Iliyokamatwa
Sep 05, 2018
Na Msemaji Mkuu

Waziri wa kilimo Mhe Dkt. Charles Tizeba akionyesha mfuko mtupu uliogushiwa na kiwanda cha Global Packaging limited wakati akizungumza na Waandishi wa Habari katika ofisi za Bodi ya Sukari Tanzania zilizopo Mtaa wa Posta Jijini Dar es salaam, Jana tarehe 2 Septemba 2018.
Waziri wa kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba (Kushoto) pamoja na Kaimu Mtendaji Mkuu Bodi ya Sukari Tanzania Ndg Miraji Kipande wakati wa mkutano na Waandishi wa Habari Jana tarehe 2 Septemba 2018 Jijini Dar es salaam.
Kaimu Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Sukari Tanzania Ndg Miraji Kipande akionyesha logo master wanayotumia katika kiwanda cha Global Packaging limited kutengenezea mifuko iliyogushiwa.
 
Na Mathias Canal, WK-Dar es salaam
 
Waziri wa kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba (Mb) ameiagiza Bodi ya Sukari Tanzania kuipima sukari yote iliyokamatwa katika mkoa wa Dar es Salaam kwa  kupitia Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA) na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) pindi kesi zinazohusiana na sukari hiyo zitakapokamilika.
 
Waziri huyo wa kilimo ametoa agizo hilo Jana tarehe 2 Septemba 2018 wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za Bodi ya Sukari zilizopo mtaa wa Posta Jijini Dar es salaam.
 
Dkt Tizeba alisema kuwa ufungashaji wa sukari kwenye ujazo wowote ule kwa kutumia vifungashio vya aina yoyote kama vile mifuko yenye nembo ya SUPER FINE lazima uzingatie Sheria ya Sukari Namba 26 ya Mwaka 2001 ambayo inazuia ufungashaji wa sukari bila kupata idhini ya Bodi ya Sukari Tanzania.
 
Alisema kuwa kwa mujibu wa Sheria hiyo ni marufuku kufungasha au kuuza sukari nyeupe kwa kuwa sukari hiyo ni kwa ajili ya matumizi ya viwandani kama malighafi na sio kwa ajili ya matumizi ya kawaida majumbani.
 
Alisisitiza kuwa Mtu yeyote atakayebainika kuvunja Sheria hiyo ya Sukari, atawajibika kulipa faini ya kiasi cha fedha kisichopungua Shilingi Milioni Kumi (10,000,000) au kifungo cha miaka mitatu (3) jela au vyote kwa pamoja.
 
Hatua hizo zimechukuliwa mara baada ya Waziri wa Kilimo Mhe. Mhandisi Dkt. Charles Tizeba (Mb) hivi karibuni kuitaka Bodi ya Sukari Tanzania kufanya ukaguzi wa maduka na maghala ya sukari kwa kushirikiana na Taasisi nyingine za Udhibiti zikiwemo Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA), Shirika la Viwango Tanzania (TBS) pamoja na Vyombo vya Ulinzi na Usalama katika mikoa ya ukanda wa Bahari ikiwemo Dar es Salaam, Pwani na Tanga pamoja na mikoa ya kanda ya ziwa hususani mkoa wa Mara.
 
Katika ukaguzi huo aina mbalimbali za sukari ya magendo zimekamatwa pamoja na mifuko tupu ambayo ni mipya ambapo watuhumiwa waliokutwa na bidhaa hizo wamefunguliwa kesi katika maeneo hayo na hatua nyingine za kisheria zinaendelea.
 
Aidha, jumla ya kilo 20 za sukari nyeupe, mifuko 106 yenye ujazo wa kilo 25 na mifuko 14 yenye ujazo wa kilo 5 za sukari ya Brown ilikamatwa katika mkoa wa Dar es Salaam ikiwa inauzwa kwenye maduka mbalimbali.
 
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Sukari Tanzania Ndg Miraji Kipande alisema kuwa jumla ya sukari yote iliyokamatwa katika mkoa wa Dar es Salaam ni kilo 2,740 (tani 2.74) huku Katika wilaya ya Bagamoyo, mfuko 1 wa sukari wenye ujazo wa kilo 50 na mifuko 3 yenye ujazo wa kilo 25 ilikamatwa. Halikadhalika katika mkoa wa Tanga mifuko 54 ya sukari ya Brown yenye ujazo wa kilo 50 ilikamatwa.
 
Kati ya mifuko ya sukari iliyokamatwa katika Mkoa wa Dar es Salaam, mifuko 106 imefungashwa kwenye mifuko yenye nembo ya Brown Sugar Product of Brazil, ambayo imebainika kuwa ni feki na imetengenezwa na kiwanda cha kutengeneza vifungashio kinachoitwa Global Packaging (T) Ltd kilichopo wilayani Kibaha. Aidha, mifuko hiyo haina taarifa sahihi za sukari iliyofungashwa kama vile tarehe iliyotengenezwa (Production Date), tarehe ya mwisho wa matumizi (expiry date) na namba ya toleo (Batch Number). Vile vile, jumla ya mifuko tupu 4,000 ya aina hiyo ambayo ni mipya ilikamatwa.
 
Kati ya mifuko hiyo, 3,000 ilikamatwa kwenye ghala la mfanyabiashara Ali Hamad Bakari lililopo Mbagala rangi tatu na mingine 1,000 ilikamatwa katika duka la mfanyabiashara Hamis Miraji Ngeruko lililopo Tandika wilayani Temeke.
 
Katika hatua nyingine kikosi kazi kilifanikiwa kukamata chapa ya kunakilishia nembo (Logo Master) ya mifuko feki ya sukari pamoja na mifuko tupu 4,500 iliyozalishwa na kiwanda cha Global Packaging (T) Ltd.
 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi