Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Dkt. Ndumbaro Ataja Manufaa ya Fedha za Mkopo kwa Wananchi wa Mkoa wa Ruvuma
Jan 04, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro amesema Wananchi wa Mkoa wa Ruvuma wana kila sababu ya kumshukuru na kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya ikiwemo kutoa fedha kwenye Wizara ya Maliasili na Utalii za kukarabati miundombinu ya maeneo ya vivutio vya utalii vilivyopo katika Mkoa huo.

Wito huo ameutoa wakati alipoongoza mamia ya wakazi wa Jimbo la Songea Mjini kwenda kusheherekea mwaka mpya wa 2022 kwa kufanya utalii wa ndani kwa nyakati tofauti katika Msitu wa Hifadhi ya Mlima Matogoro pamoja na Bustani ya Wanyamapori ya Ruhila iliyopo katikati ya Manispaa ya Songea Mjini.

Akitaja manufaa ya fedha hizo, Dkt. Ndumbaro amesema Songea ni mji uliobarikiwa kuwa na vivutio vingi vya utalii hivyo fedha hizo za mkopo zitatumika kwa ajili ya kuimarisha miundombinu ya maeneo ya vivutio ili kuimarisha utalii

Amesisitiza kuwa Hifadhi ya Msitu wa Mlima Matogoro ni kivutio kikubwa cha utalii katika mkoa huo isipokuwa changamoto ya barabara ndiyo imekuwa kikwazo cha watalii walio wengi kushindwa kufika.

Dkt. Ndumbaro amesema kupitia fedha hizo za mkopo itajengwa barabara ya uhakika itakayofika hadi juu ya misitu ya milima Matogoro ili kuwarahisishia wanaoenda kufanya utalii huku akisisitiza kuwa tayari Mkandarasi amepatikana na anatarajiwa kukabidhiwa eneo la ujenzi tarehe 15 Januari mwaka huu. 

"Mhe. Rais ametuona na kutuamini wana Songea kwa kutupatia fedha kwa ajili ya kutengeneza barabara ili kuhakikisha watalii watakaoamua kutumia magari yao kufika katika kilele cha Mlima huo wanaweza kufika tofauti na ilivyo sasa magari madogo huku hayawezi kufika kutokana na ubovu wa barabara", alisema Dkt.Ndumbaro.

Pia, Dkt. Ndumbaro amesema Mhe. Rais Samia Samia aliridhia kutengwa kwa Bajeti ya mwaka huu ya jumla ya kiasi cha shilingI milioni 50 kwa ajili ya kukarabati uzio wa Bustani ya Wanyamapori ya Ruhila.ambayo imezidi kupata umaarufu siku za hivi karibuni baada ya kufanyika kwa maboresho makubwa

Dkt. Ndumbaro amesema kuboreka kwa miundombinu katika maeneo ya vivutio vya utalii kutachochea Manispaa ya Songea mjini kimapato.kwa vile Utalii ni sekta mtambuka

Hata hivyo, Dkt. Ndumbaro amewataka wakazi wa Songea kuchangamkia fursa za utalii zilizopo katika mkoa huo huku akiwasisitiza kujenga tabia ya kutembelea maeneo ya vivutio hivyo ili kutambua fursa zilizopo kwenye maeneo yao.

Katika hatua nyingine Waziri Ndumbaro amewataka Wananchi hao kuwa mstari wa mbele kulinda na kuhifadhi maeneo ya vivutio vya utalii badala ya kuiachia Wizara pekee ili maeneo hayo yaweze kuchochea kipato kwa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla kupitia sekta ya utalii.

Katika kusherehekea sikukuu ya Mwaka Mpya katika Bustani ya Wanyamapori ya Ruhila, Waziri Ndumbaro aliweza kuwalipia wakazi wote wa Songea Mjini tozo zote za vingilio katika Bustani hiyo pamoja na kuhakikisha  wanakula nyama pori iliyokuwa imeandaliwa kwa ajili ya wakazi hao

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi