Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Dkt. Nchemba Aita Wawekezaji Kuwekeza Nchini Tanzania
Oct 16, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Benny Mwaipaja, Washington DC


Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, ametoa wito kwa wawekezaji wa kimataifa pamoja na wazawa kuchangamkia fursa za uwekezaji zinazopatikana nchini Tanzania katika sekta mbalimbali.


Dkt. Nchemba ametoa wito huo mjini Washington D.C, Marekani, alipokutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi anayesimamia masuala ya masoko ya mitaji, maendeleo ya nishati na mabadiliko ya tabianchi wa Taasisi ya Benki ya Dunia inayoshughulika na utoaji dhamana katika Uwekezaji kwa Sekta Binafsi (MIGA), Bw. Sarvesh Suri, ambapo Dkt. Nchemba anaongoza Ujumbe wa Tanzania kwenye Mikutano ya Mwaka ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF).


Alisema kuwa, Serikali inaendelea kuboresha mazingira rafiki ya uwekezaji na biashara ili kuchochea uwekezaji na kuvutia mitaji na teknolojia kutoka nje ya nchi na kuiomba taasisi hiyo itoe dhamana kwa kampuni, taasisi au mashirika yanayotaka kuwekeza nchini Tanzania.


“Tuna maeneo ya uwekezaji kwenye nishati, reli ya kisasa, kilimo, utalii na miundombinu ya barabara ambayo ni fursa kwa uwekezaji,.” alisema Dkt. Nchemba.


Dkt. Nchemba alisema kuwa Tanzania iko katika eneo la kimkakati kijiografia kwa kuwa inapakana na nchi nyingi zisizopakana na bahari na pia inajivunia uwepo wa soko la uhakika la bidhaa zitakazozalishwa katika maeneo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika SADC.


Aidha, aliiomba Taasisi hiyo ya MIGA itoe dhamana kwa wawekezaji wenye nia ya kuwekeza nchini Tanzania ili waweze kupata mikopo yenye riba nafuu ili wawekeze kwenye maeneo hayo ambayo yatawapatia faida na kukuza ajira.


Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Emmanuel Tutuba, alisema kuwa Tanzania iko katika hatua za mwisho za kurekebisha sheria ya kulinda uwekezaji ambayo ikikamilika itachochea zaidi uwekezaji.


“Tumepeleka rasimu ya sheria hiyo ya uwekezaji bungeni na hivi sasa tunakusanya maoni ya wadau na baadae itawasilishwa tena bungeni na tunatarajia sheria hiyo ikipitishwa itaondoa urasimu wa mchakato wa uibuaji miradi ya PPP na pia kulinda uwekezaji,” Alisema Bw. Tutuba.


Kwa upande wake, Mkurugenzi anayesimamia masuala masoko ya mitaji, maendeleo ya Nishati na Mabadiliko ya Tabianchi wa Taasisi ya Benki ya Dunia inayoshughulika na utoaji dhamana katika Uwekezaji kwa Sekta Binafsi (MIGA), Bw. Sarvesh Suri, aliipongeza Tanzania kwa hatua zake za kuboresha mazingira ya uwekezaji ambayo yameanza kuwavutia wawekezaji wengi wanaotaka kuwekeza nchini kupitia taasisi yake.


Alisema kuwa kongamano la uwekezaji Barani mwa frika lililofanyika Dar es Salaam tarehe 14-15 Septemba, 2022 na kuwakutanisha wadau mbalimbali wa uwekezaji kutoka ndani na nje ya Bara la Afrika kujadili fursa na changamoto za uwekezaji barani humo, umewavutia wawekezaji wengi walioonesha nia ya kuwekeza mitaji yao umeiwezesha Tanzania kujulikana na wawekezaji wengi zaidi ambao wengi wao wameonesha nia ya kuwekeza mitaji yao nchini humo hatua itakayochangia kuchochea ukuaji wa uchumi wa nchi na maisha ya  watanzania.


Bw. Suri alisema kuwa Sekta Binafsi ndiyo injini ya ukuaji wa uchumi wa nchi yoyote duniani na kwamba mazingira mazuri ya uwekezaji yanayofanywa na Tanzania kupitia mabadiliko ya sheria mbalimbali zilizokuwa zinakwaza uwekezaji wa mitaji na teknolojia nchini, yatakuza uwekezaji huo.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi