Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Dkt. Nchemba Aiasa PPRA Kuhakikisha Wazabuni Wanatumia Malighafi na Bidhaa za Ndani
Sep 28, 2024
Dkt. Nchemba Aiasa PPRA Kuhakikisha Wazabuni Wanatumia Malighafi na Bidhaa za Ndani
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu akipokea Taarifa ya Tathmini ya Utendaji Kazi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) kwa mwaka wa fedha 2023/2024 kutoka kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya PPRA, Dkt. Leonada Mwagike katika ofisi ndogo za Wizara ya Fedha jijini Dar es Salaam, 28 Septemba, 2024. Kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Bw. Dennis Simba.
Na Benny Mwaipaja, Dar es Salaam

Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu ameiagiza Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), kuhakikisha kuwa watoa huduma wanaopata zabuni kupitia Mfumo wa Ununuzi wa Kieletroniki wa NeST, wanatumia malighafi na bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi isipokuwa kwa bidhaa ambazo ni lazima ziagizwe nje ya nchi kutokana na kutopatikana hapa nchini.

 

Dkt. Nchemba, amepokea maelekezo hayo wakati akipokea Taarifa ya Tathmini ya Utendaji Kazi PPRA kwa mwaka wa fedha 2023/2024, tukio lililofanyika katika ofisi ndogo za Wizara ya Fedha jijini Dar es Salaam, 28 Septemba, 2024.

 

Dkt. Nchemba alisema kuwa hatua hiyo itakuza uzalishaji wa bidhaa na huduma za ndani, kukuza ajira, kuongeza wigo wa kodi na kuchangia maendeleo ya nchi kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali inayotekelezwa na Serikali. 

 

Aidha, Dkt. Nchemba amezitaka taasisi za umma nchini kuhakikisha zinatumia Mfumo wa Ununuzi wa Umma wa Kielektroniki (NeST) kwa kuwa hakuna mbadala wake.


Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wawakilishi wa Menejimenti ya Wizara ya Fedha, baada ya Waziri wa Fedha kupokea Taarifa ya Tathmini ya Utendaji Kazi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), kwa mwaka wa fedha 2023/2024, kutoka kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya PPRA, Dkt. Leonada Mwagike, katika ofisi ndogo za Wizara ya Fedha jijini Dar es Salaam, 28 Septemba, 2024. , walioketi kulia ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bi. Amina Khamis Shaaban (Usimamizi wa Fedha za Umma), Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha (Huduma za Hazina), Bi. Jenifa Christian Omolo na kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa PPRA, Bw. Dennis Simba na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya PPRA, Dkt. Leonada Mwagike. 

 

Alisema kuwa matumizi ya Mfumo huo yanaongeza uwazi na uwajibikaji na udhibiti wa ndani wa taasisi nunuzi na hivyo kuendana na maelekezo ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, aliyeitaka Wizara ya Fedha kudhibiti matumizi ya fedha za Serikali hasa kwenye utekelezaji wa miradi ili iendane na thamani ya fedha inayotumika kutekeleza miradi husika.

 

Akizungumza wakati wa kukabidhi Taarifa hiyo. Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka hiyo, Dkt. Leonada Mwagike, alisema kuwa Taasisi yake inajivunia mafanikio makubwa ikiwemo kufanikisha maboresho ya Sheria ya Ununuzi wa Umma ya Mwaka 2023 na kanuni zake za Mwaka 2024. 

 

Alisema kuwa katika kutekeleza majukumu yake ya ukaguzi na usimamizi wa Sheria za Ununuzi wa Umma, PPRA ilifanikiwa kuokoa kiasi cha shilingi bilioni 14.94 kupitia ukaguzi na kiasi kingine cha shilingi trilioni 2.7 wakati wa ufuatiliaji wa mipango kazi ya Ununuzi wa taasisi nunuzi iliyowasilishwa katika taasisi hiyo na kubainika kuwa matumizi hayo hayakuwa na tija. 

 

Aidha, alisema kuwa PPRA iliwezesha ushiriki wa makundi maalum, yakiwemo ya wanawake, vijana, watu wenye mahitaji maalum kunufaika na zabuni 153 zenye thamani ya shilingi bilioni 5.29.

 

Ripoti hiyo imekabidhiwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya PPRA, Dkt. Leonada Mwagike na kushuhudiwa na Naibu Makatibu Wakuu wa Wizara ya Fedha, Bi. Jenifa Christian Omolo na Bi. Amina Khamis Shaaban, Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya PPRA, baadhi ya Menejimenti ya Wizara ya Fedha, wafanyakazi wa PPRA na wageni wengine waalikwa.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi