Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Dkt. Mwakyembe Aipongeza MCL Kusimamia maadili
Aug 22, 2017
Na Msemaji Mkuu

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe akibofya kitufe kuashiria uzinduzi rasmi wa Muonekano Mpya wa Gazeti la Michezo la Mwanaspoti Jijini Dar es Salaam. Wanaoshuhudia tukio hilo ni baadhi ya Viongozi waandamizi wa Kampuni ya Uchapishaji Magazeti ya Mwananchi Communications Ltd (MCL).

Na. Benedict Liwemba-WHUSM

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe ameipongeza Kampuni ya Uchapishaji Magazeti ya Mwananchi Communications Limited (MCL) kwa jitihada kubwa wanazozifanya katika kusimamia maadili kwa kuhabarisha na kuielimisha jamii ya Kitanzania.

Pongezi hizo amezitoa jana wakati wa Uzinduzi wa Muonekano Mpya wa gazeti pendwa la michezo la Mwanaspoti linalochapishwa na Kampuni hiyo.

Dkt. Mwakyembe amesema kuwa, mara kwa mara MCL imekuwa ikiisaidia jamii kwa kujihusisha katika masuala mbalimbali ya kijamii kama vile wakati wa tetemeko la ardhi Mkoani Kagera imeweza kutoa mchango wake mkubwa kwa jamii na daima imekuwa ikilinda maadili na weledi wa kazi ya uandishi kwa wafanyakazi wake jambo ambalo linaonyesha ushirikiano mzuri baina ya Serikali, Kampuni na jamii.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe akichomoa gazeti jipya la Michezo la Mwanaspoti ambalo lina muonekano mpya wa kisasa zaidi mara baada ya kulizindua Jijini Dar es Salaam.

“Mimi nawapongeza na kuwashukuru sana MCL kwakuwa mstari wa mbele katika kulinda maadili katika kazi zenu, endeleeni kulinda maadili kwa kuhabarisha na kuielimisha jamii, sijaona mkivunja maadili ya kazi zenu na hakika mnajijengea sifa nzuri kwa wengine”, alisema Dkt. Mwakyembe.

Aliongeza kuwa, kwa sasa kumeibuka wimbi kubwa la Waandishi wa habari (Makanjanja) ambao hawana vyeti wala weledi wa kufanya kazi ya uandishi wa habari na hao wamekuwa kila wakati wakirusha taarifa zisizo sahihi hususani katika mitandao ya kijamii jambo ambalo Serikali haiwezi kulifumbia macho.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa MCL, Bw. Francis Nanai amesema kwamba lengo la kampuni hiyo kuja na muonekano mpya wa gazeti hilo ni kuwapa ladha mpya wasomaji wake nchini kote, na hiyo ni mara ya sita kwa gazeti hilo kubadilishwa muonekano wake tangu kuanzishwa kwake mwaka 2001.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya  Mwananchi Communications Ltd (MCL), Bw. Francis Nanai (kulia) wakiwaonesha Waandishi wa habari muonekano mpya wa gazeti la michezo la Mwanaspoti mara baada ya uzinduzi Jijini Dar es Salaam.

“Sisi kama wadau wa michezo tumewasikiliza wasomaji wa gazeti letu na tukayafanyia kazi mawazo yao na ndiyo maana tukaamua kuja na muonekano mpya wa gazeti hili ambao uko kimataifa zaidi”, alisema Nanai.

Aliongeza kuwa, gazeti hilo lilianzishwa likiwa na waandishi wa tatu tu mwaka 2001 na lilikuwa likitoa nakala 3,000 kwa siku ambapo kwa sasa kuja kwa muonekano mpya wa gazeti hilo kutaongeza idadi ya wasomaji tofauti ilivyokuwa mwanzo na idadi ya uchapishaji imeongezeka hadi kufikia nakala 60,000 kwa siku.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe akiongea na wageni waalikwa, Viongozi wa Kampuni ya  Mwananchi Communications Ltd (MCL) pamoja na Waandishi wa habari wakati wa uzinduzi wa Muonekano Mpya wa Gazeti la Michezo la Mwanaspoti Jijini Dar es Salaam.

(Picha na Benedict Liwemba-WHUSM)

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi