Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Dkt. Mpango Aweka Jiwe la Msingi Kiwanja cha Ndege Tabora
Oct 09, 2024
Dkt. Mpango Aweka Jiwe la Msingi Kiwanja cha Ndege Tabora
Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango akivuta kitambaa kuashiria uwekaji wa jiwe la msingi la upanuzi na ukarabati wa Kiwanja cha Ndege cha Tabora Oktoba 9, 2024 mkoani Tabora.
Na Wizara ya Ujenzi

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango ameweka jiwe la msingi mradi wa ujenzi na upanuzi wa kiwanja cha ndege Tabora na kuzipongeza Wizara za Ujenzi na Uchukuzi kwa kazi nzuri wanayoifanya katika mradi huo. 

 

Akizungumza wakati wa hafla hiyo Oktoba 9, 2024, Dkt. Mpango amezitaka  Wizara hizo kushirikiana kikamilifu ili mradi huo ukamilike kwa wakati na thamani ya fedha ionekane.

Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi, Godfrey Kasekenya akitoa taarifa ya mradi wa upanuzi na ukarabati wa Kiwanja cha Ndege cha Tabora, Oktoba 9, 2024 mkoani Tabora wakati wa hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la mradi huo.

"Tambueni kuwa fedha hizi ni za wananchi hivyo zitumike vizuri kwa maendeleo ya wananchi", amesisitiza Dkt. Mpango.

 

Aidha, kuhusu usalama barabarani, Dkt. Mpango ametoa rai kwa madereva na watumiaji wa vyombo vya moto nchini kuzingatia alama za barabarani ili kuepusha ajali na kuwaonya wale wanaohujumu alama za barabarani kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

 

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya amesema ukarabati na upanuzi wa kiwanja hicho umefikia asilimia 72 huku  jengo la abiria likiwa na uwezo wa kuhudumia abiria 120 kwa wakati mmoja litakapokamilika.

Muonekano wa ujenzi wa jengo la abiria katika Kiwanja cha Ndege cha Tabora ambao ujenzi wake unaendelea.

"Mheshimiwa Makamu wa Rais, mradi huu pia unahusisha barabara ya kuruka na kutua ndege, mnara wa kuongozea ndege, barabara za maingilio na maegesho ya ndege na barabara ya kuingia katika kiwanja cha ndege, maegesho ya magari, uzio wa usalama na kituo cha hali ya hewa", amefafanua Mhandisi Kasekenya.

 

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Kasekenya amesema Serikali itaendelea kuunganisha barabara za lami katika mikoa ya magharibi ili ifikike kwa urahisi na kuchochea shughuli za uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara na hivyo kukuza uchumi wa wananchi.

 

Naye, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), Mhandisi, Mohamed Besta amesema ujenzi wa kiwanja hicho unatekelezwa na mkandarasi Beijing Construction Engineering Group Co, kutoka China kwa gharama ya shilingi bilioni 24.6.

 

Kiwanja cha ndege cha Tabora kilianzishwa mwaka 1940 na kimekuwa kikiboreshwa mara kwa mara na kukamilika kwake kutawezesha ndege nyingi kubwa kukitumia kiwanja hicho na kuchochea shughuli za kijamii na kiuchumi katika Mkoa wa Tabora na ukanda wa magharibi kwa ujumla.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi