Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Dkt. Mpango Awataka Wana Tanga Kutunza Mazingira ili Kulinda Miundombinu
Feb 21, 2024
Dkt. Mpango Awataka Wana Tanga Kutunza Mazingira ili Kulinda Miundombinu
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Isdor Mpango akipunga mkono wakati akizungumza na wananchi wa Kabuku wilayani Handeni katika ziara yake mkoani Tanga.
Na Ofisi ya Makamu wa Rais

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Isdor Mpango amewataka wananchi wa Mkoa wa Tanga kutunza na kulinda mazingira kwa kuepuka vitendo vya ukataji miti hovyo na uchomaji wa misitu hali inayoharibu uoto wa asili na kusababisha uharibifu wa miundombinu ya barabara.

Akizungumza na wakazi wa Kabuku wilayani Handeni, Dkt. Mpango amesema uharibifu wa mazingira unaathiri uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara mkoani Tanga kwani unasababisha ukame na mvua nyingi zisizo na msimu na hivyo kuharibu barabara.

“Hakikisheni mnatunza na kulinda mazingira ili kupunguza athari za mabadiliko ya tabia nchi na hivyo kurejesha thamani ya mkoa wa Tanga katika uzalishaji wa mazao hususan mahindi, matunda na mboga za majani amesisitiza Dkt. Mpango.

Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya akizungumza na wananchi katika ziara ya Makamu wa Rais, Dkt. Philip Isdor Mpango Kabuku mkoani Tanga.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya amemhakikishia Makamu wa Rais kuwa Wizara kupitia Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Tanga umejipanga kuhakikisha barabara ya Handeni –Mafuleta Km 20 ujenzi wake unaendelea kwa kasi ili kufidia muda uliopotea kutokana na changamoto za Mkandarasi.

Aidha, Mhandisi Kasekenya amesema kuhusu kuunganisha Mkoa wa Tanga na Morogoro kupitia barabara ya Handeni-Mziha-Turiani km 108.2, tayari kibali cha ujenzi huo kimepatikana na ujenzi wake utaanza hivi karibuni kwa kuanza na kipande cha Km 30.

Amezitaja barabara za nyingine zinazoendelea kujengwa mkoani Tanga kuwa ni barabara ya Tanga-Pangani, Pangani-Mkaja-Mkange km 120.8 na kusisitiza kuwa usanifu wa barabara ya Mkata-Kwamsisi Km 36 unaendeelea ili nayo ijengwe kwa lami.

“Mheshimiwa Makamu wa Rais Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi inatarajia kuanza usanifu wa kupanua barabara ya Chalinze-Segera ambayo ilijengwa muda mrefu ili kuiboresha na kuiwezesha kuhudumia wasafiri na wasafirisjhaji kwa tija”, amesisitiza Naibu Waziri Kasekenya.

Dkt. Mpango amesisitiza umuhimu wa wakazi wa mkoa huo kuhakikisha wanawapeleka watoto wao shule na kuhakikisha wanapa lishe bora ili kuwa na taifa la watu wasomi na wenye akili na afya njema.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi