Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Dkt. Mpango Atoa Wito Watanzania Kumuenzi Mwl. Nyerere
Oct 14, 2023
Dkt. Mpango Atoa Wito Watanzania Kumuenzi Mwl. Nyerere
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango akizungumza kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Misa Maalum ya Kitaifa ya Kumuombea Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere iliyofanyika katika Kanisa Katoliki Parokia ya Roho Mtakatifu – Babati mkoani Manyara.
Na Ofisi ya Makamu wa Rais

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa Watanzania kumuenzi Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa kufanya kazi kwa bidii ili kuboresha maisha pamoja na kuinua uchumi wa Taifa.

Makamu wa Rais amesema hayo wakati akizungumza kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Misa Maalum ya Kitaifa ya Kumuombea Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere iliyofanyika katika Kanisa Katoliki Parokia ya Roho Mtakatifu – Babati mkoani Manyara.

Amewasihi viongozi na Watanzania kwa ujumla kumuenzi Baba wa Taifa kwa kuishi katika misingi ya kukemea rushwa, kupiga vita umasikini, kutojilimbikizia mali pamoja na kukemea matendo mabaya. Vile vile, Makamu wa Rais amewasihi viongozi wa dini kuendelea kuliombea taifa amani na utulivu.

"NI wajibu kwa Watanzania kumuenzi kwa kuishi maisha aliyoishi Baba wa Taifa kwa kuwa alitumia elimu na vipaji vyake kwa faida ya wote, alithamini dhamana aliyopewa, alikuwa mnyenyekevu na mwenye kujisahihisha alipokosea, alikemea matendo mabaya yaliyochochea mmomonyoko wa maadili, alikuwa mwanamazingira hodari na alipiga vita umasikini", alisema Dkt. Mpango.

Aidha, Makamu wa Rais amelishukuru Kanisa pamoja na taasisi zingine za kidini kwa ushirikiano wake na Serikali kwa kutoa huduma mbalimbali za kijamii kama vile elimu, afya, mazingira na mengineyo. Amesema Serikali itaendelea kushirikiana vema na Kanisa Katoliki pamoja na madhehebu yote ya dini katika kuwatumikia Watanzania.

Misa Maalum ya Kitaifa ya Kumuombea Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere imeongozwa na Askofu wa Jimbo Katoliki la Mbulu, Anthony Lagwen na kuhudhuriwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, viongozi mbalimbali pamoja na waumini kutoka maeneo mbalimbali nchini.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi