Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Dkt. Mpango Akagua Upanuzi Barabara ya TANZAM
Aug 02, 2023
Dkt. Mpango Akagua Upanuzi Barabara ya TANZAM
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango akizungumza baada ya kukagua barabara ya mchepuo wa Inyala yenye kilometa 2.8 na upanuzi wa barabara ya TANZAM sehemu ya Inyala - Shamwengo yenye kilometa 3 mkoani Mbeya.
Na Mwandishi Wetu

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango amekagua barabara ya mchepuo wa Inyala yenye kilometa 2.8 na upanuzi wa barabara ya TANZAM sehemu ya Inyala - Shamwengo yenye kilometa 3 mkoani Mbeya.

Akizungumza wakati wa ukaguzi wa barabara hiyo uliofanyika jana Makamu wa Rais, Dkt. Mpango ameipongeza Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) kwa kazi kubwa waliyofanya ya ujenzi wa barabara katika eneo hilo ambalo lilipoteza maisha ya watu wengi kutokana na ajali za mara kwa mara.

“Madereva wa vyombo vya moto kote nchini wawe waangalifu kuendesha vyombo vya usafiri, kujenga utaratibu wa kukagua usalama wa magari yao wenyewe na kuzingatia sheria ili wanaowaendesha waendelee kuwa salama na kuepuka madhara yatokanayo na ajali zitokanazo na uzembe wa madereva barabarani”, alisema Mhe. Dkt. Mpango.

Muonekano wa barabara ya mchepuo wa Inyala yenye kilometa 2.8 na upanuzi wa barabara ya TANZAM sehemu ya Inyala - Shamwengo yenye kilometa 3 mkoani Mbeya.

Dkt. Mpango aliwataka askari wa usalama barabarani kusimamia sheria kikamilifu lakini isiwe ndio kisingizio cha wao kutafuta fedha za mfukoni na badala yake wafanye kazi yao kwa uadilifu.

Akitoa taarifa fupi ya mradi huo, Meneja wa TANROADS mkoa wa Mbeya Mhandisi Matari Masige alisema kuwa ujenzi wa barabara hiyo ulitokana na agizo la Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango tarehe 12 Septemba 2022, alipotembelea eneo hilo na kuiagiza Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kupitia TANROADS waimarishe barabara hiyo kwa kiwango cha lami, kupanua sehemu ya Mlima Inyala na pia kuweka taa sehemu za kukagulia magari kabla ya kuteremka na kupanda mlima.

Aliongeza kuwa kufuatia agizo hilo, Serikali iliidhinisha bajeti ya dharura kwa ajili ya kufanya ujenzi kwa kiwango cha lami, ambapo mradi huo umegharamiwa na Serikali ya Tanzania kwa asilimia 100 na umetekelezwa na Mkandarasi China Geo - Engineering Corporation kwa gharama ya shilingi bilioni 6.999 kwa kusimamiwa na TANROADS mkoa wa Mbeya.

Aidha Inyala ni eneo lenye mteremko mkali katika barabara kuu ya TANZAM mkoani Mbeya uliopelekea kutokea matukio ya mara kwa mara ya ajali za barabarani ambazo zilisababisha madhara mbalimbali ikiwemo vifo na majeruhi kwa watumiaji wa barabara hiyo.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi