Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Dkt Mpango Akabidhi Hatimiliki za Kimila Makete
Oct 27, 2023
Dkt Mpango Akabidhi Hatimiliki za Kimila Makete
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt Philip Isdori Mpango akikabidhi Hatimiliki za Kimila kwa wananchi wa Makete mkoa wa Njombe wakati wa ziara yake ya siku tatu mkoani humo tarehe 27 Oktoba 2023. Katikati ni Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geofrey Pinda.
Na Munir Shemweta, WANMM MAKETE

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdori Mpango amekabidhi Hati ya Hakimiliki za Kimila kwa wananchi wa Wilaya ya Makete Mkoa wa Njombe.

 

Dkt. Mpango amekabidthi hati saba za mfano kati ya Hatimiliki za Kimila 6,883 zilizoandaliwa tarehe 27 Oktoba, 2023 katika halfa iliyofanyika  Kijiji cha Tandala wilayani humo akiwa katika ziara yake ya kikazi ya siku tatu katika Mkoa wa Njombe.

 

Akizungumza mbele ya Makamu wa Rais, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Geofrey Pinda amesema, utolewaji Hati za Kimila wilayani Makete unafuatia uwezeshwaji uandaaji mipango ya matumizi bora ya ardhi uliofanywa na wizara yake kupitia Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi katika vijiji.

 

Kwa mujibu wa Mhe. Pinda, Mkoa wa Njombe una jumla ya vijiji 323 ambapo vijiji 264 kati ya hivyo tayari vimewezeshwa kuandaliwa mpango wa matumizi bora ya ardhi.

 

"Mhe. Makamu wa Rais Mkoa wa Njombe tunavyo vijiji 323 na kati ya hivyo vijiji 295 tayari vimewezeshwa na sasa tuko katika Wilaya ya Makete kama taarifa ilivyoeleza", alisema Mhe. Pinda.

 

Awali Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Makete, Bw. William Makufwe amesema kuwa, upatikanaji wa Hatimiliki hizo ni jitihada za Wilaya kukuza zao la ngano àlilolieleza kuwa linazalishwa kwa wingi katika Wilaya hiyo.

 

Aidha, Mkurugenzi huyo ameeleza kuwa, Wilaya yake imeamua kuendesha kilimo cha zao hilo kimkakati kwa kupima na kumilikisha mashamba kupitia Hatimiliki za Kimila ili ziwape fursa wakulima ya kuongeza mitaji itakayoinua wigo wa uzalishaji zao hilo.

 

Ugawaji wa Hatimiliki hizo unafuatia kazi iliyofanywa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kupitia Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi iliyowezesha uandaaji wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Vijiji 64 katika wilaya ya Makete na kutoa jumla ya Hatimiliki za Kimila 6,889.

 

Kazi hiyo imetekelezwa katika awamu mbili ambapo, awamu ya kwanza, ilihusisha uandaaji mipango ya matumizi ya ardhi katika vijiji 44 na upimaji wa vipande vya ardhi katika vijiji 17 ambapo jumla ya hati 6,594 ziliandaliwa.

 

Aidha, katika awamu ya pili uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji 20 kwenye Tarafa ya Ukwama na Lupalilo ulifanyika ambapo vijiji 20 viliwezeshwa kuandaa  mipango ya matumizi ya ardhi na hati miliki za kimila 287. 

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi