Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Dkt. Mahenge Awataka Wakandarasi Kumaliza Miradi ya Madaraja Kabla Msimu wa Mvua Haujafika
Aug 10, 2021
Na Jacquiline Mrisho

Mkuu wa Mkoa Singida, Mhe. Dkt. Binilith Mahenge amewataka TANROAD kumaliza haraka ujenzi wa daraja unaoendelea katika Kata ya Msingi Wilayani Mkalama Mkoani humo ili kurahisisha mawasiliano katika maeneo mbalimbali  kabla msimu wa mvua haujaanza.

Dkt. Binilith Mahenge ametoa maelekezo hayo leo tarehe 10.08.2021 alipotembelea mradi wa ujenzi wa daraja lililopo   Kata ya Msingi wilaya ya Mkalama ambapo amesema daraja hilo likikamilika litaweza kuhudumia mikoa ya Mwanza Simiyu na Manyara.

Aidha, amewapongeza viongozi wa TANROAD mkoani hapo kwa usimamizi mzuri wa ujenzi huo na kuwataka kuhakikisha kwamba daraja linakamilika kwa ubora na muda uliopangwa.

Hata hivyo Mkuu wa Mkoa huyo amebainisha kwamba kumalizika kwa ujenzi wa daraja hilo utagharimu kiasi cha shilingi bilioni 10.9 na linatakiwa kukamilika ifikapo Octoba 30, 2020.

Aidha, Mhe. Dkt. Mahenge amewapongeza viongozi wa TANROAD kwa usimamizi mzuri pamoja na changamoto za mvua kwa msimu uliopita lakini kazi imeendelea kuwa nzuri.

Amesema kukamilika kwa daraja hilo kutahamasisha kwa kiasi kikubwa ukuaji wa uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

“Nimefahamishwa kwamba dararaja hili linaunganisha mikoa ya Simiyu, Mwanza, Manyara na kwa Mkoa wa Singida linaunganisha Wilaya ya Mkalama na Iramba, ni matumaini yangu kwamba shughuli za uchumi zitaimarika sana kwa mtu mmoja na Taifa kwa ujumla wake”, alisema Dkt. Mahenge.

Awali akimkaribisha RC, Mkuu Wilaya ya Mkalama Mhe.  Sophia Mfaume Kizigo amesema daraja hilo ambalo ni kiungo muhimu cha wilaya hiyo na Iramba litawasaidia wananchi wa maeneo hayo kuendesha shughuli za kila siku kwa ufasaha kutoka eneo moja kwenda jingine.

Aidha, ufanikishwaji wa daraja hilo utasababisha barabara nyingine zinazounga wilaya na mikoa mbalimbali kujengwa kwa kiwango cha lami alisisitiza Mhe.  Sophia

Naye Diwani wa Kata ya Msingi wilayani hapo, Mhe. Amri Juma  ameishukuru Serikali kwa jitihada za kufanikisha ujenzi wa daraja hilo na mengine madogo yanayojengwa na TARURA katika Kata hiyo kwamba ni ishara ya mabadiliko makubwa ya kiutendaji unaofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita.

Naye Mhandisi Deus Masige, Meneja wa TANROAD mkoani Singida amesema daraja lina urefu wa mita 100 na midomo ya kupitisha maji  mnne ambapo limefikia asilimia 67 na linatumia fedha za ndani.

Ujenzi wa daraja hilo ulitegemewa kumalizika   Disemba 11/12, 2021 lakini kutokana na changamoto za mvua kwa msimu uliopita halikuweza kumalizika kwa wakati.

Mhandisi Masige amehakikishia Mkuu wa Mkoa huyo kwamba pamoja na changamoto zilizojitokeza lakini ujenzi wa daraja hilo utakamilika kwa muda uliopangwa.

Katika hatua nyingine, Mhe. Dkt. Binilith Mahenge amewataka wananchi wa Mkalama na maeneo mengine kujikinga na ungojwa wa UVIKO19 na kuendelea kupata chanjo ambazo Serikali imeshazisambaza maeneo mbalimbali mkoani hapo.

Amesema Mkoa umepokea chanjo zaidi ya 30,000 ili wananchi waweze kupata  chanjo hizo ambazo serikali imejiridhisha kwamba ni salama kwa afya ya watu wake.

Aidha, Mhe. Dkt. Mahenge amewaagiza Wakuu wa Wilaya zote mkoani hapo kuendelea kuhamasisha wananchi kupata chanjo hiyo kama sehemu ya mapambano dhidi ya ugonjwa huo.

Amewataka Madiwani kusaidia kutoa elimu kwa wananchi kuhusu misongamono ambayo sio ya lazima ili kuepuka usambazaji wa ugonjwa huo endapo mtu mmoja atakuwa ameathirika.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi