Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Dkt. Kalemani Asema Corona Isiwe Kisingizio cha Kutokamilisha Miradi ya Umeme
Mar 27, 2020
Na Msemaji Mkuu

Na Zuena Msuya, Geita

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani amewataka wakandarasi wanaotekeleza miradi ya usambazaji wa umeme vijijini, kujikinga na kuchukua tahadhari dhidi ya virusi vya Corona ili kuendelea kutekeleza miradi hiyo na kuikamilisha kwa wakati unaotakiwa kwa mujibu wa mikataba.

Dkt. Kalemani alisema hayo, Machi 26, 2020, wakati akiwasha umeme katika Kituo cha Afya cha Bwina, kuwasha taa za barabarani zinazotumia mwanga wa jua ( Solar) na kuwahamasisha wananchi kuendelea kuchukua tahadhari na kujikinga dhidi ya virusi vya Corona katika Wilaya ya Chato mkoani Geita.

Dkt. Kalemani alisema kuwa tishio dhidi ya kuwepo kwa virusi vya Corona kusirudishe nyuma juhudi za utekelezaji wa miradi ya usambazaji umeme vijijini kwa kuwa tayari mamlaka husika zimetoa miongozo ya kujikinga na kujihadhari dhidi ya virusi hivyo katika maeneo mbalimbali nchini.

“Tujikinge na tuchukue tahadhari dhidi ya Corona, kazi ya kusambaza umeme vijijini lazima iendelee tena kwa kasi ya hali ya juu na miradi ikamilishwe kwa wakati uliopangwa, cha muhimu ninyi wakandarasi kufuata miongozo iliyotolewa na mamlaka husika ili muweze kutekeleza majukumu yenu, lazima tufanye kazi tusambaze umeme, wananchi wanataka umeme uwake,” alisema Dkt.Kalemani.

Aliendelea kuwasisitiza wakandarasi kutotumia kisingizio cha kuwepo virusi vya Corona kuchelewesha ama kutokamilisha miradi ya kusambaza umeme vijijini pamoja na ujenzi wa mradi mkubwa wa kufua umeme kwa kutumia maji wa Mwalimu Nyerere.

Alisema mamlaka husika zimeweka wazi na kuendelea kutoa matangazo kila kona ya nchi hii ya namna bora ya kujikinga na kuchukuwa tahadhari dhidi ya virusi vya Corona, hivyo wakandarasi katika maeneo yao ya kazi kuhakikisha wanasimamia na kutekeleza miongozo hiyo.

Akizindua na kuwasha taa za barabarani katika mitaa ya Wilaya Chato mkoani Geita, Dkt.Kalemani alisema kuwa lengo la kuweka taa hizo ni kuongeza usalama kwa wananchi wanaotumia barabara hizo nyakati za usiku.

Aidha Dkt. Kalemani aliwasha umeme katika Kituo kipya cha afya cha Bwina wilayani humo ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za afya wakati wote kwa wagonjwa wanaofika kutibiwa katika kituo hicho.

Dkt. Kalemani aliwataka wananchi kulinda miundombinu ya taa hizo pamoja na kuitunza ili idumu kwa muda mrefu kwa faida yao na kuwahimiza wananchi kwenda kutibiwa wakati wote katika kituo cha afya cha Bwina.

Katika ziara hiyo ,vilevile aliwasisitiza wananchi kuendelea kutekeleza maagizo na maelekezo yanayoendelea kutolewa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto na wadau mbalimbali wa afya ya kujikinga dhidi ya Virusi vya Corona, ikiwemo kunawa mikono mara kwa mara, kuepuka misongamano na mikusanyiko na kutoa taarifa pale tu wanapomuona mtu mwenye dalili za ugonjwa huo kama zinavyoelezwa katika matangazo.

Dkt. Kalemani alikuwa akifanya ziara yake hiyo pasipo kuwa na mikutano ya kuzungumza na wananchi, kusimama umbali mrefu kati yake na baadhi ya watu alioambatana nao, vyombo vya habari na kunawa mikono kila baada ya kufika eneo husika na kupaka kitakasa mikono (Sanitizer) ili kujikinga dhidi ya virusi vya Corona.

Ikumbukwe kuwa Machi 24, 2020, katika Mkutano wa Baraza la Mawaziri, Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa alielekeza kuwa sehemu kubwa ya ziara ya Mawaziri katika kutekeleza majukumu yao, iwe ni kuwahamasisha wananchi kuendelea kuchukua tahadhari na kujinga dhidi ya virusi vya Corona, kwa kufuata njia bora na sahihi zinazotolewa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi