Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Dkt. Jafo Apokea Taarifa Mashirika Yanayofadhili Miradi ya Mazingira, Mabadiliko Tabianchi
Oct 09, 2023
Dkt. Jafo Apokea Taarifa Mashirika Yanayofadhili Miradi ya Mazingira, Mabadiliko Tabianchi
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Mhe. Dkt. Selemani Jafo akifanya mazungumzo na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa yanayofadhili miradi ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi inayotekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini.
Na Mwandishi Wetu

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Mhe. Dkt. Selemani Jafo amekutana na kufanya mazungumzo na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa yanayofadhili miradi ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi inayotekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini.

Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika leo Oktoba 9, 2023 katika Ofisi ndogo za Ofisi Makamu wa Rais Jijini Dar es Salaam, Waziri Jafo amepokea taarifa kutoka kwa wawakilishi hao kuhusu uwasilishaji wa andiko la taarifa la vipaumbele miradi ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi itakayowasilishwa katika Baraza la Mfuko wa Mazingira wa Dunia (GEF) mwishoni mwa mwezi huu.

Waziri Jafo amesema kikao hicho na wawakilishi wa mashirika hayo sehemu ya ufuatiliaji wa maazimio ya Mkutano Mkuu wa Saba wa GEF uliofanyika katika Mji wa Vancouver nchini Canada, ambapo nchi zilizoendelea na zinazoendelea zilikubaliana kuwezesha ukusanyaji wa fedha katika shughuli za uhifadhi wa mazingira duniani.

Amesema Tanzania bado ina mahitaji makubwa ya rasilimali fedha kutoka GEF kwa ajili ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, hivyo mara baada ya kumalizika kwa kwa mkutano huo Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais iliunda timu ya wataalamu kwa ajili ya kupitia vipaumbele vya miradi ya mazingira na mabadiliko ya tabia nchi kwa ajili ya uratibu wa maombi ya fedha za utekelezaji na usimamizi wa miradi hiyo.

“Tanzania ni mhanga mkubwa wa mabadiliko ya tabianchi. Leo ukitazama Wilaya ya Simanjiro utaona ni kwa jinsi gani wafugaji wanavyohangaika na mifugo. Si hapo tu na Mpwapwa napo hali nayo si nzuri. Hivyo tunahitaji miradi mingi zaidi ya ufadhili wa fedha ili kuzinusuru jamii zetu,” amesema Waziri Jafo.

Kwa upande wake Mshauri wa Rais, masuala ya Mabadiliko ya Tabianchi na Mazingira Dkt. Richard Muyungi ameyashukuru mashirika hayo kwa kuendelea kufadhili miradi mbalimbali ya mazingira hapa nchini na kuongeza kuwa mahitaji makubwa zaidi ya fedha bado yanahitaji ili kuleta manufaa kwa jamii na taifa kwa ujumla.

Akitolea mfano Dkt. Muyungi amesema Serikali imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi ikiwemo ujenzi wa mradi wa kingo za bahari ya Hindi katika maeneo ya barabara ya Barack Obama (Ocean Road) ambao umelenga kuzuia mmomonyoko wa udongo baharini.

Dkt. Muyungi amesema Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali yakiwemo mashirika ya kimataifa ili juhudi za pamoja ziendelee kuimarishwa katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kuhakikisha miradi ya uhifadhi na usimamizi wa mazingira inaendelea kuibuliwa katika jamii.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP), Bi. Clara Makenya amesema Shirika hilo litaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuhakikisha juhudi za pamoja zinaendelea kuchukuliwa katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi ikiwemo ufadhili wa miradi na uwezeshaji wa fedha.

“Katika andiko letu UNEP tutakalowasilisha GEF tumeainisha maeneo mapya ya miradi kwa Tanzania. Tayari tuna miradi katika maeneo matano. Tumepanga kuangalia awamu ijayo tuanze kuitekeleza Zanzibar na maeneo ya Mikoa ya Nyanda za Juu kusini” amesema Bi. Makenya.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi