Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Dkt. Chaula Akabidhiwa Ofisi Rasmi na Dkt. Jingu
Jan 21, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na WMJJWM Dodoma

Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Zainabu Chaula amekabidhiwa rasmi Ofisi ya Wizara na aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Afya Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii ambaye kwa sasa ni Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Dkt. John Jingu.

Makabidhiano hayo yamefanyika katika Ofisi za Wizara jijini Dodoma baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, kuiunda Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum.

Akizungumza katika hafla ya makabidhiano hayo, Katibu Mkuu wa Wizara, Dkt. Zainabu Chaula amewataka watumishi wa Wizara hiyo kutimiza majukumu yao kwa ufanisi na kujituma katika kutekeleza majukumu yao.

"Kila mmoja hapa ana karama yake, sasa tuunganishe hayo maarifa ya mtu mmoja mmoja tutembee pamoja", Dkt. Chaula.

Ameongeza kuwa, kiongozi ni wasifu katika eneo analofanya kazi na kuleta matokeo chanya kwenye eneno la utekelezaji wa majukumu yao hivyo, ni vyema kuhakikisha wanatumia vipawa vyao kusadia kutatua changamoto zilizopo katika jamii.

"Tutumie ujuzi na uwezo wote tulionao kuhakikisha tunasaidiana katika kutekeleza majukumu yetu kwa ufanisi na ufasaha ili kuleta matokeo chanya" alisema Dkt. Zainabu Chaula.

Kwa upande wake, aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Afya Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii ambaye ni Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Dkt. John Jingu amewashukuru Watumishi wa Wizara hiyo mpya kwa ushirikiano waliompa wakati akitekeleza majukumu yake na kuwaasa kuendelea kuwapa ushirikiano viongozi wapya katika utekelezaji wa majukumu waliyopewa na Rais.

"Nawaahidi nitaendelea kuwapa ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu yenu tuendelee kutekeleza majukumu yetu kwa ufanisi ili kumsaidia Rais katika kutatua changamoto za kimaendeleo", alisema Dkt. Jingu

Akizungumza katika hafla hiyo, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Amon Mpanju, amewaasa watumishi kupendana na kushirikiana kwa pamoja katika majukumu yao ili kuwasaidia Viongozi kuendeleza jukumu la Maendeleo.

Mapema Januari 8, 2022, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe Samia Suluhu Hassan, aliunda Wizara mpya ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum na kisha kuteuwa Viongozi wa kuingoza Wizara hiyo.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi