Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ameiagiza Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kuhakikisha barabara inayokwenda mlimani kulipojengwa mitambo ya Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), wilayani Ngorongoro, mkoani Arusha inapitika wakati wote.
Mhe. Dkt. Biteko amesema hayo leo Aprili 15, 2024 wilayani Ngorongoro, mkoani Arusha wakati akizindua vituo vinne vya kurushia matangazo ya TBC Taifa na Bongo FM wilaya za Ngorongoro (Arusha), Uvinza (Kigoma), Makete (Njombe) na Kyela (Mbeya). Uzinduzi huo ni kiashiria cha kuelekea miaka 60 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Nimeambiwa zipo changamoto za barabara kwenda kwenye kituo chetu, naomba niwaagize TARURA na Mhe. Mkuu wa Mkoa pamoja na TARURA wilaya, hakikisheni barabara inayokwenda mlimani, inapitika wakati wote,” amesema Mhe. Dkt. Biteko.
Amesema kuwa, mabilioni ya fedha yaliyowekwa katika kituo hicho, kama hakuna barabara itayowafikisha wataalam huko, mitambo inaweza kuharibika na isitengenezwe na kuwa hasara kwa nchi.
Kuhusu changamoto ya umeme ya kuwa na laini ya njia moja katika kituo hicho, Dkt. Biteko amewaambia TBC kupeleka maombi ili wapeleke laini ya njia tatu kwa ajili ya kuwapelekea umeme na kuacha kutegemea jenereta ambayo gharama yake ni kubwa.
Kwa upande wake, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye amesema Shirika la Utangazaji Tanzania linaendelea kuboresha matangazo yake kwa sababu linatambua kwamba lina jukumu la kuhabarisha taifa letu, katika kuliunganisha, kuchochea maendeleo na kuwafanya watu wapambane kujiletea maendeleo yao wenyewe.
“Mwaka 2021 wakati Dkt. Samia Suluhu Hassan anaingia madarakani, matangazo ya shirika letu yalikuwa yanakwenda wilaya 119 ambayo ilikuwa ni sawa na asilimia 74, miaka mitatu baadaye tumefika wilaya 158 ambayo ni asilimia 92 ya ‘coverage’ ya nchi nzima, na uzinduzi wa leo unaenda kuongeza,” amesema Mhe. Nape.
Aidha, amesema kuwa, lengo la Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi, kufikia mwakani, ni nchi nzima wawe wanasikia matangazo kutoka Shirika la Utangazaji Tanzania.