Na Shamimu Nyaki
Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Hassan Abbasi amefunga Warsha ya Uhamasishaji wa Uzalishaji na Usambazaji wa Maudhui bora ya ndani, leo Septemba 16, 2022 Jijini Dar es Salaam ambayo imeandaliwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).
Dkt. Abbasi amefunga Warsha hiyo kwa Niaba ya Waziri wa wizara hiyo, Mhe.Mohamed Mchengerwa, ambapo amesisitiza Waandaaji wa Maudhui kuzingatia Mila, Desturi, Utamaduni na matumzi sahihi ya Lugha ya kiswahili katika Maudhui hayo.
"Wizara inaendelea kusisitiza uzalishaji wa Maudhui bora yanayozingatia Mila na Desturi za Tanzania katika eneo la Sanaa na Utamaduni kwa kuwa ndio utambulisho wa Taifa letu", alisema Dkt. Abbasi.
Katibu Mkuu Abbasi amewataka wadau wa Maudhui kutanguliza ajenda za kitaifa wanapokua wanazalisha na kutangaza maudhui kwa walaji.
Amesisitiza matumizi ya maneno yenye staha na kuepuka dhihaka hasa katika maudhui ya mitandaoni ambayo jamii haifurahishwi nayo, huku akisisitiza hakuna uhuru bila mipaka.
Aidha, ameahidi wizara yake itashirikiana na TCRA katika maazimio yote yaliyofikiwa katika warsha hiyo na ipo tayari kutoa ushirikiano katika maeneo ya utoaji wa Tuzo kwa Wazalishaji Bora wa Maudhui kwa kuwa imefanikiwa katika eneo la kuandaa Tuzo za filamu na Muziki.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dkt. Jabir Bakari amesema Warsha hiyo imetoa maoni na mapendekezo bora katika kuzalisha na kusambaza maudhui ya ndani.