Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Dkt. Mpango Kuongoza Mkutano wa Kudhibiti Utakasaji Fedha Haramu
Aug 28, 2017
Na Msemaji Mkuu

Na: Mwandishi Wetu

Waziri wa Fedha na Mipango Dk. Philip Mpango anatarajiwa kuongoza kikao cha siku mbili cha Baraza la Mawaziri la Nchi za Umoja wa Mashariki na Kusini mwa Afrika la Kudhibiti Utakasishaji wa Fedha Haramu (ESAAMLG) utakaofanyika Zanzibar, kuanzia tarehe 8 Septemba, 2017.

Katika mkutano huo, Serikali itawasilisha taarifa ya utekelezaji wa Mpango wa Kimataifa wa Kushughulikia Udhibiti wa Utakasishaji Fedha Haramu (The Financial Action Force-FATF).

Mpango huo ambao ulianzishwa mwaka 2008 unazitaka nchi wanachama kufanya tathmini ya utekelezaji wa maazimio yaliyopitishwa na FATF katika maeneo ya kisheria, kisera, miongozo ya kitaasisi zikiwemo sekta za fedha na ushirikiano wa kimataifa.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na Wizara ya Fedha na Mipango kwa vyombo vya habari, hatua hiyo inakusudia kubainisha jinsi nchi wanachama zilivyojidhatiti kushughulikia suala la utakasaji fedha haramu na ufadhili wa ugaidi katika nchi zao.

Katika mkutano huo, wajumbe watajadili mbinu na mikakati mbalimbali za kudhibiti tatizo la utakasaji fedha haramu na ufadhili wa ugaidi hatua ambayo inatarajiwa kuleta matokeo yatakayosaidia kuchangia kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi katika nchi wanachama.

Tanzania ambayo ni mwenyekiti wa umoja huo kwa sasa, ni miongoni mwa wanachama waanzilishi wa umoja huo ambao sasa una wanachama 18 kutoka wanachama waanzilishi 7.

Wanachama hao ni Afrika Kusini, Angola, Botswana, Ethiopia, Kenya, Lesotho, Madagascar, Malawi, Mauritius, Msumbiji, Namibia, Rwanda, Swaziland, Seychelles, Tanzania,  Uganda, Zambia na Zimbabwe.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, vikao vya maandalizi ya mkutano huo vitakavyohusisha maafisa waandamizi wa nchi wanachama vinatarajiwa kufanyika kwa siku nne kuanzia tarehe 2 Septemba hadi 6 Septemba katika hoteli ya Zanzibar Beach Resort.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi