Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

DC Uyui Asisitiza Uwazi na Uwajibikaji wakati wa Kutekeleza Miradi ya Maendeleo
Nov 05, 2018
Na Msemaji Mkuu

Na ; Mwandishi wetu- Uyui

Viongozi wa  Wilaya ya Uyui wametakiwa kutoa taarifa ya mapato na matumizi ya fedha zinazochangiwa na wananchi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Kata zote za Wilaya hiyo.

Akizungumza katika Kijiji cha Songambele kilichopo Kata ya Miyenze, Mkuu wa Wilaya hiyo  Mhe. Gift Issaya Msuya amesema kuwa wananchi wanayohaki ya kujua mapato na matumizi ya miradi ya maendeleo wanayochangia ili kuongeza tija katika kutekeleza miradi  hiyo.

"Kuanzia sasa mimi niko Wilaya ya Uyui nisije nikasikia kwamba mnafanya mambo bila ya kuwashirikisha wananchi, mmechangisha michango, mmeanza kutekeleza miradi ya maendeleo ni lazima muwashirikishe wananchi kwa kutoa taarifa ya mapato na matumizi na kila hatua inayofikiwa katika utekelezaji wa mradi  husika"; Alisisitiza Msuya.

Akifafanua amesema kuwa wananchi wanapaswa kupata taarifa ya kila jambo katika maeneo yao na huo ndio utawala Bora unaosisitiza uwazi na uwajibikaji kwa wananchi.

Agizo hilo litaongeza kasi ya maendeleo katika Kata zote za Wilaya hiyo na hivyo kuendana na kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano inayosisitiza Viongozi kuwajibika katika kuwaletea wananchi maendeleo.

Kwa upande wake Mtendaji wa Kata ya Miyenze Samweli  Manyika  ameahidi kuwa watafanyia kazi maelekezo yote yaliyotolewa na Mkuu wa Wilaya hiyo wakati wa ziara yake katika Kata hiyo iliyolenga kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika miradi ya maendeleo katika maeneo yao hasa kuwepo kwa uwazi na uwajibikaji.

Aliongeza kuwa wataongeza kasi yakutoa taarifa kwa wananchi kuhusu miradi ya maendeleo  ambayo wananchi wamekuwa wakichangia fedha na rasilimali mbalimbali ili kuchochea maendeleo katika maeneo yao.

Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Songambele Bw. Shaban Mingili amesema kuwa atasismamia utekelezaji wa agizo hilo la kutoa taarifa ya mapato na matumizi ya miradi ya maendeleo kama ilivyoagizwa.

Mkuu wa Wilaya ya Uyui amekuwa akisisitiza uwazi na uwajibikaji  kwa viongozi wa katika ngazi zote katika Wilaya hiyo ili kuendana na azma ya Serikali ya Awamu ya Tano inayosisitiza uwazi na uwajibikaji katika kuwaletea wananchi maendeleo.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi