Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

DC Nyamagana Akoshwa na Mradi wa Maji Butimba
Aug 26, 2023
DC Nyamagana Akoshwa na Mradi wa Maji Butimba
Muonekano wa ujenzi wa mradi wa maji Butimba unaotekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) ambao kwa sasa umefikia asilimia 94 ya utekelezaji wake.
Na Na Mwandishi Wetu

Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Mhe. Amina Makilagi  amefurahishwa na kasi ya utekelezaji wa mradi wa maji Butimba unaotekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) baada ya mradi kufikia asilimia 94 ya utekelezaji hadi sasa.

Ameyasema hayo Agosti 26, 2023 wakati wa ziara ya kukagua mradi eneo la Butimba ambapo ameeleza kufurahishwa na maendeleo ya mradi huku akieleza kwamba hatua iliyopigwa ni kubwa.

"Tunawashukuru na kuwapongeza MWAUWASA kwa utendaji wao wa kazi nzuri, kwa kipindi kifupi tumeona mabadiliko makubwa katika utekelezaji. Kwa kasi hii tunapata matumaini kwamba utekelezaji utakamilika ndani ya muda na huduma itapatikana kama ilivyokusudiwa," amesema Mhe. Amina.

Aidha, Mhe. Amina ameiagiza MWAUWASA kuhakikisha inafanya kazi ndani ya muda uliopangwa ili kupunguza changamoto ya upatikanaji wa maji kwa wananchi.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MWAUWASA, Bi. Neli Msuya amepokea maelekezo hayo na kuahidi kuendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa mradi.

Akizungumzia hatua iliyofikiwa ya utekelezaji wa mradi, Bi.  Neli ameeleza kwamba kwa ujumla mradi umefikia asilimia 94 na kwamba kazi za ujenzi ziko katika hatua za mwisho.

"Hadi sasa kasi ya utekelezaji ni ya kuridhisha, sasa tunafanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha tunakamilisha kila hatua na tutafanya majaribio tarehe 15/9/2023 kama ilivyopangwa," amesema Bi. Neli.

Mradi wa Maji Butimba unatekelezwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Benki ya Uwekezaji ya Ulaya na Shirika la Maendeleo la Ufaransa kwa gharama ya shilingi bilioni 69.

Kukamilika kwa mradi kutaboresha na kuwezesha upatikanaji huduma ya majisafi kwa wakazi wapatao 450,000 waishio maeneo ya pembezoni.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi