Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

DAWASA Yatumia zaidi ya Milioni 230 Kuimarisha  Huduma za Maji Temeke
Jul 05, 2018
Na Msemaji Mkuu

Frank Mvungi.

Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar-es-Salaam (DAWASA) imetumia kiasi cha Shilingi Milioni 239.1 kuboresha uzalishaji wa maji katika mtambo wa kusukuma maji uliopo eneo la Mtoni wilayani Temeke, Jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa iliyosambazwa kwenye vyombo vya habari imeeleza kuwa kiasi hicho cha fedha kimetumika kuweka mashine mbili za kusukuma maji ghafi kutoka mto Kizinga ambazo zinatarajiwa kusukuma kiasi cha mita za ujazo 280 kwa saa.

Kufungwa kwa pampu hizo kutaongeza upatikanaji wa maji ghafi kutoka mto Kizinga kwenda kwenye mtambo wa Mtoni na hivyo kurejesha uwezo wa mtambo huo kuzalisha maji kwa ufanisi kwa ajili ya matumizi ya wakazi na viwanda kwenye eneo lote la Temeke linalohudumiwa na DAWASA.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo mtambo wa Mtoni ulijengwa miaka ya 1947 ukiwa na uwezo wa kuzalisha lita milioni tisa na kuhudumia maeneo machache ya manispaa ya Temeke. Hata hivyo, kwa sasa mtambo wa Mtoni unahudumia maeneo ya Tandika, Mtoni kwa Azizi Ally, Mtongani na baadhi ya vitongoji vya kata za Kurasini, Mtoni Kijichi na Mbagala.

Aidha, Taarifa hiyo imebainisha kuwa vyanzo vingine vya maji vilivyopo kwa ajili ya eneo la huduma la DAWASA na ambavyo kwa ujumla huzalisha maji lita milioni 502 kwa siku ni pamoja na; Mtambo wa Ruvu Juu uliozinduliwa kwa mara ya kwanza mwaka 1956 na baadae kupanuliwa na kuzinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli Juni 21, 2018.

Vyanzo vingine ni visima virefu vilivyopo katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam vikilenga kuimarisha huduma za maji kwa wananchi wote.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi