Na; Mwandishi Wetu
Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASA) imefanikiwa kuvutia mamia ya Wakazi wa Jiji la Dar es Salaam kuomba kurejeshewa huduma ya maji safi baada ya huduma hiyo kusitishwa hapo awali kutokana na wateja hao kushindwa kulipa madeni ya ankara za maji kwa kipindi kilichopita.
Kwa mujibu wa Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka hiyo Mhandisi Cyprian Luhemeja amesema kuwa wananchi wote waliokatiwa maji kwa muda mrefu wanatakiwa kufika katika Ofisi za DAWASA zilizopo katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam na Viunga vyake pamoja na Kibaha na Bagamoyo Mkoani Pwani ili taratibu za kuwarejeshea maji zifanyike.
Akizungumzia lengo la Mamlaka hiyo Mhandisi Luhemeja amesema kuwa ni kuhakikisha kuwa inaongeza wateja na pia kuwarejesha wale waliokatiwa maji kwa muda mrefu baada ya kushindwa kulipa bili zao ambapo sasa wataingia makubaliano maalum na Mamlaka hiyo yatakayowawezesha kupata huduma ya maji na kuendelea kulipa deni kidogo kidogo kulingana na makubaliano hadi watakapomaliza madeni yao.
Hatua zinazochukuliwa na Mamlaka hiyo katika kuboresha huduma zake ni pamoja na kuvutia wateja wapya na kurejesha wale waliokatiwa maji kwa muda mrefu.
Sehemu ya Taarifa ya Mamlaka hiyo kupitia mtandao wake wa kijamii wa Tweeter inasema kuwa wananchi wameonesha mwitikio mkubwa katika maeneo yote yanayohudumiwa na DAWASA hasa kwa kuwasilisha maombi ya kurejeshewa huduma hiyo.
“ Kutoka mkoa wa Kinondoni wateja zaidi ya 50 wamejitokeza kuomba kurejeshewa huduma ya maji safi na salama hivyo ni mwanzo mzuri kutokana na mwitikio huu ambao umeonesha wazi kuwa wananchi wanaunga mkono juhudi za Serikali kuhakikisha wanafikiwa na huduma bora”; inasisitiza sehemu ya taarifa ya Mamlaka hiyo.
Hatua nyingine zinazochukuliwa na Mamlaka hiyo ni pamoja na kudhibiti mivujo ya maji, kufikisha huduma ya maji maeneo ya pembezoni na pia kuhakikisha kuwa maeneo ya viwanda yanafikiwa na huduma hiyo ili kuchochea uchumi wa viwanda.DAWASA imekuwa ikitekeleza miradi yakimkakati inayolenga kuhakikisha kuwa wananchi wote wanafikiwa na huduma ya majisafi na salama katika Jiji la Dar es Salaam na Pwani tangu Mamlaka hiyo ilipoundwa upya baada kuvunjwa kwa DAWASCO hivi karibuni na majukumu yake kuhamishiwa DAWASA.