Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

COSTECH Yaendelea Kufadhili Miradi ya Kimkakati
Aug 26, 2023
COSTECH Yaendelea Kufadhili Miradi ya Kimkakati
Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, Dkt. Amos Nungu akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Tume hiyo na mwelekeo wa utekelezaji kwa Mwaka wa Fedha 2023/24 jijini Dodoma kwenye ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO) leo Agosti 24, 2023.
Na Immaculate Makilika – MAELEZO

Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) imeendelea kuratibu, kukuza na kuendeleza miradi utafiti kwa kutekeleza shughuli mbalimbali.

Akizungumza jana jijini Dodoma, Mkurugenzi Mkuu wa Tume hiyo, Dkt. Amos Nungu wakati  akieleza utekelezaji wa majukumu ya Tume na mwelekeo wa utekelezaji kwa mwaka wa fedha 2023/2024 amesema kuwa Serikali kupitia COSTECH imeidhinisha jumla ya miradi saba  yenye thamani ya shilingi milioni 150  kila mradi. Ambapo miradi hiyo itatekelezwa  ndani ya miaka miwili itahusisha watafiti na wabunifu kutoka sekta zote za umma na binafsi.

“Miradi mingi ya utafiti hufadhiliwa kwa kipindi cha miaka miwili hadi mitatu. Kwa sasa ipo miradi kadha inayoendelea na ipo hatua mbalimbali ambayo Serikali ilifadhili kupitia COSTECH. Michache katika miradi hiyo ya utafiti inayoendelea katika hatua mbalimbali za utekelezaji na Tume inafanya ufuatiliaji ni pamoja na ile inayohusu kuboresha maabara za utafiti kwa ukarabati na ununuzi wa vifaa vya kisasa”, ameeleza Dkt. Nungu.

Dkt. Nungu ametaja baadhi ya miradi hiyo ni  kuwa ni Maabara ya Utafiti wa Baharini katika Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA) inayolenga kuboresha mazingira ya utafiti katika uchumi wa bluu na kuwa mradi huo ulikamilika kwa kasi sana na kuzinduliwa mnamo tarehe 11 Aprili, 2023.

Aidha, Maabara ya chanjo ya mifugo katika Taasisi ya Taifa ya Chanzo (TVLA) iliyopo Kibaha. Vifaa hivyo vimeiwezesha TVLA kuwa na uwezo wa kuhakiki ubora wa chanjo zinazozalishwa na kutoa ithibati ya chanjo hizo kuweza kushindana katika soko la Kikanda na Kimataifa.

“Mradi wa Maabara ya afya ya Udongo ya Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA). Vifaa vinawezesha upimaji wa Udongo kulingana na zao husika na hivyo kuongeza uzalishaji katika sekta ya kilimo. Mathalani kiwanda cha Sukari Mtibwa kimeanza kutumia Maabara hii kuhakiki aina ya Udongo katika uzalishaji wa zao la miwa”, amefafanua Dkt. Nungu.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi