Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Albert Chalamila, amezindua ufanyaji biashara kwa saa 24 katika soko la Kariakoo jijini Dar es Salaam, na kuwahakikishia wafanyabiashara ulinzi na usalama kwenye eneo hilo.
Katika uzinduzi huo uliofanyika usiku wa Februari 27, 2025 kwenye soko la kimataifa Kariakoo na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwepo mabalozi pamoja na wasanii wa muziki na filamu, Chalamila aliwataka wananchi wa mkoa huo na nchi jirani zinazofanya biashara na kariakoo, kuunga mkono ufanyikaji wa biashara saa 24 na kuongeza kuwa, Dar es Salaam ina miundombinu ya kutosha kuhudumia wafanyabiashara hao kwa muda huo wa usiku.
“Dar es Salaam tuna hospitali nzuri za kisasa, tuna barabara nzuri, tuna bandari, tuna kituo cha mabasi cha kimataifa cha Magufuli, tuna reli ya kisasa ya SGR, tuna jeshi imara la polisi, TRA, vyote hivi vinatoa huduma saa 24, kwa hiyo wafanyabiashara tuchape kazi”,amesema Chalamila.
Amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alitoa maelekezo kuhusu soko la Kariakoo kufanya kazi saa 24, ili kwenda kasi na maendeleo ulimwenguni ambapo nchi nyingi wanafanya saa 24.
Aidha, RC Chalamila amesema Mataifa yaliyoendelea hufanya biashara saa 24 na kupanua wigo wa ajira kwa vijana, hivyo kwa kuwa mkoa huo ni kitovu cha biashara, kwa kufanya hivyo vijana watapata fursa za kujiajiri na TRA pia itaweza kukusanya mapato mengi zaidi.
Amewahakikishia wafanyabiashara usalama wa kutosha, na kwamba Dar es Salaam ni salama sana na miundombinu ya kiusalama inaendelea kuimarishwa ikiwemo kuwekwa taa na kamera katika mitaa.
Aidha, amesema baada ya uzinduzi huo ataunda kamati itakayoongozwa na Katibu Tawala wa Mkoa, Dkt. Toba Nguvila kwa ajili ya kupitia sheria zinazokinzana na kufanya biashara saa 24, hasa sheria ndogo ndogo za Halmashauri za Manispaa ambapo pia ameyataja maeneo mengine yatayofungua soko saa 24 kuwa ni pamoja na Mwenge, Manzese ,Tandika,Mbagala,Ubungo na Magufuli Bus Stand.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es salaam, Dkt.Toba Nguvila amesema kuwa pamoja na kuruhusiwa kufanyika kwa biashara kwa saa 24 bado kamera hazijafungwa ambapo zoezi la ufungaji katika soko hilo unatarajiwa kuanza Machi 1 mwaka huu.
"Tayari tumeshasaini mkataba na TEMESA kufunga kamera 40 katika awamu ya kwanza ambapo tumetenga bajeti. Kwa upande wa taa TARURA wanatarajia kufunga taa 700 na kazi ya ufungaji itaanza muda wowote kuanzia sasa". Amesema Toba.