Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

BMT Kuandaa Muongozo Kuhusu Ukomo wa Wachezaji wa Nje Nchini
Apr 30, 2020
Na Msemaji Mkuu

[caption id="attachment_52370" align="aligncenter" width="750"] Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Michezo wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Yusuph Singo akifafanua kuhusu usajili wa wanamichezo wa kigeni hapa nchini leo Aprili 29,2020 Jijini Dodoma.[/caption]

Na Shamimu Nyaki, WHUSM-Dodoma

Baraza la Michezo la Taifa (BMT) limepewa jukumu la kuendelea kuandaaa mwongozo utakaotumika kukusanya maoni kutoka kwa wadau kuhusu ukomo wa wanamichezo wa nje hapa nchini.

Hayo yamesemwa leo Jijini Dodoma na Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Michezo Bw.Yusuph Singo kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ikiwa ni hatua ya kuboresha na kuimarisha sekta ya michezo nchini.

Bw. Singo amesema kuwa Serikali haijatoa ukomo wa wachezaji kutoka nje kushiriki michezo hapa nchini bali imeibua mjadala kwa wadau ili watoe maoni yao.

“Katika Hotuba ya Bajeti iliyosomwa hivi karibuni Bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe, hakuongelea idadi ya wachezaji kutoka nje wanaotakiwa kucheza nchini, bali aliagiza BMT kuandaa mjadala mpana katika kukusanya maoni kwa wadau wa michezo kuhusu namna bora ya kusajili wachezaji wa kigeni katika michezo yote hapa nchini”, alisema Bw. Singo.

Pamoja na hayo, Mkurugenzi huyo ambainisha kuwa Mhe.Waziri Dkt. Mwakyembe alisisitiza kuwa wanamichezo wote kutoka nje ya nchi wanaosajiliwa hapa nchini ni lazima wawe na ubora pamoja na viwango vinavyotakiwa.

Akifafanua suala hilo Bw. Singo amesema kuwa michezo yote ya kulipwa kwa sasa imeendelea kukua duniani kote na nchi yetu pia inayo wachezaji wengi wanaocheza michezo hii ikiwemo Mpira wa Kikapu (Basketball), Kriketi, Mpira wa Miguu na michezo mingine, hivyo, Serikali haijatoa maelekezo ya ukomo wa usajili wa idadi ya wachezaji bali inataka kuwepo kwa mjadala wa wazi utakaotoa mwongozo wa ukomo wa idadi ya usajili wa wachezaji wa kigeni.

Aidha, Mkurugenzi huyo alitoa rai kwa wadau wa michezo nchini watakapopata fursa ya kuchangia au kutoa maoni katika mjadala huo wasiegemee katika timu wanazoshabikia, bali watoe maoni ambayo yatasaidia kuendeleza michezo na kuendeleza vipaji vya wanamichezo wetu pamoja na kukuza michezo nchini.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi