Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Bilioni 743 Zatolewa kwa Wanufaika Milioni 6 - Waziri Mkuu
Apr 15, 2024
Bilioni 743 Zatolewa kwa Wanufaika Milioni 6 - Waziri Mkuu
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akihitimisha hoja ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, taasisi zake, na mfuko wa Bunge kwa mwaka 2024/2025, bungeni jijini Dodoma, Aprili 15, 2024.
Na Ofisi ya Waziri Mkuu

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema katika mwaka 2023/2024, shilingi bilioni 743.7 zimetolewa kwa wanufaika zaidi ya milioni sita kupitia mifuko na programu za uwezeshaji wananchi kiuchumi.

 

Ameyasema hayo leo jioni (Jumatatu, Aprili 15, 2024) bungeni, jijini Dodoma wakati akitoa hoja ya kuhitimisha mjadala wa bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Taasisi zake na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2024/2025.

 

“Serikali imeendelea kutekeleza sera mbalimbali za uwezeshaji wa makundi maalum ya wanawake, vijana na wenye ulemavu. Lengo likiwa ni kuhakikisha makundi haya yanashiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi hapa nchini.” 

 

Amesema katika kutekeleza sera ya ushirikishwaji wa Watanzania kwenye miradi ya kimkakati na uwekezaji nchini, wanawake na vijana wameendelea kunufaika kupitia miradi ya kimkakati na uwekezaji ambapo katika mwaka 2023/2024, Watanzania 162,968 wamenufaika na ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja. 

 

“Serikali imeendelea kuratibu masuala ya uzalishaji wa fursa za ajira nchini kwa kujenga mazingira wezeshi kwa wawekezaji na kuimarisha ushirikiano baina ya serikali na sekta binafsi. Katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita, fursa za ajira 2,489,136 zimezalishwa sawa na wastani wa ajira mpya 829,712 kwa mwaka,” amesema. 

 

Kuhusu vijana, Waziri Mkuu Majaliwa amesema serikali imeendelea kuwawezesha vijana ili waweze kujiari, kushiriki kwenye shughuli za maendeleo na kuchangia katika Pato la Taifa. “Katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita, shilingi bilioni 3.19 kimetolewa kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana ambazo zilitumika kutoa mikopo ili kuwezesha miradi 148 katika sekta za kilimo, viwanda na biashara katika halmashauri 62.” 

 

Amesema serikali imetoa mafunzo ya ujasiriamali, usimamizi, kurasimisha na kuendeleza biashara kwa vijana katika maeneo mbalimbali nchini ambapo hivi karibuni, Ofisi ya Rais - TAMISEMI itatoa taarifa ya mfumo utakaotumika kutoa mikopo ya asilimia 10 kutoka Halmashauri nchini.

 

Katika hatua nyingine, akisisitiza umuhimu wa kuhifadhi mazingira, Waziri Mkuu amesema kuwa athari za uharibifu wa mazingira ni mbaya kwa kuwa huathiri masuala ya kijamii na kiuchumi.

 

“Mara kadhaa tumeshuhudia vifo vya mifugo kutokana na ukame na uhaba wa maji vilivyotokana na mabadiliko ya tabianchi yaliyosababishwa na uharibifu wa mazingira. Vilevile, mvua nyingi kupita kiasi zimeendelea kusababisha athari kubwa nchini ikiwemo mafuriko, vifo na uharibifu wa miundombinu mbalimbali.”

 

Kutokana na umuhimu wa uhifadhi wa mazingira, Waziri Mkuu ametoa maagizo matano kwa viongozi nchini ambayo yanawataka viongozi wote kuanzia ngazi ya vijiji hadi mikoa wasimamie kikamilifu uhifadhi wa mazingira na suala hili liwe ajenda ya kudumu katika vikao vyao.

 

Pia amewataka viongozi wa Mikoa na Wilaya wasimamie utoaji wa elimu kwa wananchi kuhusu athari za kuchoma misitu hovyo, kufuga bila kuangalia uwezo wa maeneo ya kulishia, kufanya shughuli za kilimo kwenye maeneo yaliyohifadhiwa na kuondokana na tabia ya kukata miti hovyo.

 

Aidha, amezitaka Halmashauri zote nchini zisimamie kikamilifu sheria ndogo za uhifadhi wa mazingira na kuwachukulia hatua watu wote wanaofanya uharibifu wa mazingira.

 

“TFS na Halmashauri ziandae vitalu vya miti inayoendana na ikolojia ya maeneo yao, kuigawa kwa wananchi, kuhakikisha inapandwa na kukua. Hatua hii iende sambamba na kusimamia upandaji wa miti kwa kila kaya. Vilevile,TANROADS na TARURA wahakikishe wakandarasi wanapanda miti pembeni mwa kila mradi wa ujenzi wa barabara.”

 

Pia amewataka wananchi waendelee kushirikiana na serikali katika uhifadhi wa mazingira ili kuepusha madhara yatokanayo na uharibifu wa mazingira katika nchi yetu. 

          

Kwa mwaka 2024/2025, Bunge limeidhinisha shilingi 350,988,412,000/- ambapo kati ya fedha hizo, shilingi 146,393,990,000/- ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi 204,594,422,000/- ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo kwa Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake.

 

Vilevile, Bunge limeidhinisha shilingi 181,805,233,000/- kwa ajili ya Mfuko wa Bunge ambapo shilingi 172,124,423,000/- ni za matumizi ya kawaida na shilingi 9,680,810,000/- ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi